Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Yohana

Yohana 12

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alienda Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye alimfufua kutoka katika wafu.
2Basi wakamwandalia chakula cha jioni huko, na Martha akamtumikia, wakati huo Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu.
3Kisha Mariamu akachukua ratli ya manukato yaliyotengenezwa kwa nardo safi, yenye thamani kubwa, akampaka Yesu miguuni, na kumfuta miguu kwa nywele zake; nyumba yote ilijaa harufu ya manukato.
4Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi wake, ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
5“Kwanini manukato haya yasingeuzwa kwa dinari mia tatu na wakapewa maskini?”
6Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini, bali kwa sababu alikuwa mwizi: yeye ndiye aliyeshika mfuko wa fedha na alikuwa anachukua baadhi ya vilivyowekwa humo kwa ajili yake mwenyewe.
7Yesu alisema, “Mwache aweke alicho nacho kwa ajili ya siku ya maziko yangu.
8Maskini mtakuwa nao siku zote; lakini hamtakuwa nami siku zote.”
9Basi umati mkubwa wa Wayahudi walipata kujua ya kuwa Yesu yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili ya Yesu tu, ila wamwone na Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka katika wafu.
10Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri ili wamue Lazaro;
11maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walienda zao na wakamwamini Yesu.
12Na siku ya pili yake umati mkubwa walikuja kwenye sikukuu. Waliposikia ya kuwa Yesu anakuja Yerusalemu,
13walichukua matawi ya miti ya mitende na kutoka nje kwenda kumlaki na wakapiga kelele, “Hosana! Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli.”
14Yesu alimpata mwana-punda akampanda; kama vile ilivyoandikwa,
15“Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.”
16Wanafunzi wake hawakuyaelewa mambo haya hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kuwa mambo haya aliandikiwa yeye na ya kwamba wametenda mambo haya kwake.
17Basi lile kundi la watu waliokuwepo pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, wakashuhudia kwa wengine.
18Na ilikuwa kwa sababu hii pia kwamba kundi la watu walikwenda kumlaki kwasababu walisikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo.

19Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, “Tazama, sasa hamwezi kufanya lolote; tazama, ulimwengu umekwenda kwake.”
20Sasa baadhi ya Wayunani walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakienda kuabudu kwenye sikukuu.
21Hawa walimwendea Filipo, ambaye alitoka Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba wakisema, “Bwana, sisi tunatamani kumwona Yesu.”
22Filipo akaenda akamwambia Andrea; Andrea na Filipo wakaenda na kumwambia Yesu.
23Yesu akawajibu akasema, “Saa imefika kwa ajili ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
24Amini, amini, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, itazaa matunda mengi.
25Yeye apendaye uhai wake ataupoteza; bali yeye auchukiaye uhai wake katika ulimemngu huu atausalimisha hata uzima wa milele.
26Mtu yeyote akinitumikia mimi, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Mtu yeyote akinitumikia, Baba atamheshimu.
27Sasa roho yangu imefadhaika: nami nisemeje? 'Baba, uniokoe katika saa hii'? Lakini ni kwa kusudi hii nimeifikia saa hii.
28Baba, ulitukuze jina lako.” Kisha sauti ikaja kutoka mbinguni na kusema, “Nimelitukuza nami nitalitukuza tena.”
29Basi mkutano uliosimama karibu naye wakasikia, wakasema ya kwamba kumekuwa ngurumo. Wengine walisema, “Malaika amesema naye.”
30Yesu akajibu na kusema, “Sauti hii haikuja kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
31Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo: Sasa mkuu wa ulimwngu huu atatupwa nje.
32Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.”
33Aliyanena hayo akionesha ni mauti gani atakayokufa.
34Mkutano wakamjibu, “Sisi tumesikia katika sheria ya kwamba Kristo atadumu hata milele. Nawe wasemaje, 'Mwana Adamu lazima ainuliwe juu'? Huyu Mwana wa Mtu ni nani?”
35Basi Yesu akawaambia, “Nuru ingalipo pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru, ili kwamba giza lisije likawaweza. Yeye aendaye gizani hajui aendako.
36Mngali mnayo nuru, iaminini nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Yesu aliyasema haya na kisha akaenda zake akajificha wasimwone.

37Ingawa Yesu alifanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, bado hawakumwamini
38ili litimie neno la nabii Isaya, alilosema: “Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?”
39Ndio sababu wao hawakuamini, maana Isaya alisema tena,
40“Amewapofusha macho, na ameifanya migumu mioyo yao; wasije wakaona kwa macho yao na wakafahamu kwa mioyo yao, na wakaongoka nami nikawaponya.”
41Isaya alisema maneno hayo kwa kuwa aliuona utukufu wa Yesu na akanena habari zake.
42Walakini, hata wakuu wengi walimwamini Yesu; lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakukiri ili wasije wakatengwa na sinagogi.
43Walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu.
44Yesu akapaza sauti na kusema, “Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi tu bali na yeye aliyenituma mimi,
45naye anionaye mimi anamuona yeye aliyenituma.
46Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.
47Ikiwa mtu yeyote atayasikia maneno yangu lakini asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, bali niuokoe ulimwengu.
48Yeye anikataye mimi na asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye: neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.
49Maana mimi sikunena kwa nafsi yangu tu. Bali ni Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.
50Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi - kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo kwao.”