12Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?”
13Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!”
14Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.
15Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?
16Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
17Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
18Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu.
19Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
20jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
21Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.
22“Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua.