Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 4

Luka 4:14-30

Help us?
Click on verse(s) to share them!
14Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.
15Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.
16Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.
17Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:
18“Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa,
19na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.”
20Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.
21Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo.”
22Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”
23Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: Mganga jiponye mwenyewe, na pia mtasema: Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako.”
24Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake.
25Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.
26Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni.
27Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria.”
28Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.
29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.
30Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.

Read Luka 4Luka 4
Compare Luka 4:14-30Luka 4:14-30