Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Yohana - Yohana 1

Yohana 1:15-45

Help us?
Click on verse(s) to share them!
15Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.”
16Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
17Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
18Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
19Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: “Wewe u nani?”
20Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”
21Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”
22Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”
23Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana.”
24Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?”
26Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
27Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”
28Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
29Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!
31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.”
32Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
33Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
34Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
35Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
36Alipomwona Yesu akipita akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu.”
37Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?”
39Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo).
42Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa.” (maana yake ni Petro, yaani, “Mwamba.”)
43Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
45Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, “Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.”

Read Yohana 1Yohana 1
Compare Yohana 1:15-45Yohana 1:15-45