1Waambie ndugu zenu wanaume, 'Watu wangu!' na kwa dada zako, 'umeonyeshwa huruma.'”
2Leteni mashtaka dhidi ya mama yenu, leteni mashtaka, kwa kuwa yeye si mke wangu, wala mimi si mumewe. Na auondoe uzinzi wake mbele yake, na matendo yake ya uzinzi kati ya matiti yake.
3Ikiwa sio, nitamvua nguo na kumuonyesha uchi wake kama siku aliyozaliwa. Nami nitamfanya kama jangwa, kama nchi iliyoharibika, nami nitamfanya afe kutokana na kiu.
4Sitakuwa na rehema kwa watoto wake, kwa maana wao ni watoto wa ukahaba.
5Maana mama yao amekuwa kahaba, na yeye aliye mimba amefanya mambo ya aibu. Alisema, “Nitawafuata wapenzi wangu, kwa maana wananipa mkate wangu na maji, sufu yangu na kitani, mafuta yangu na kinyweji.”
6Kwa hiyo nitajenga ua wa kuzuia njia yake kwa miiba. Nitajenga ukuta dhidi yake ili asiweze kupata njia. Yeye atawafuatilia wapenzi wake, lakini yeye hatawafikia.
7Yeye atawatafuta, lakini hatawapata. Kisha atasema, “Nitarejea kwa mume wangu wa kwanza, kwa maana ilikuwa ni bora kwangu zamani kuliko sasa.”
8Kwa maana hakujua kwamba mimi ndimi niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta, na ambaye nilimwongezea fedha na dhahabu, ambazo walizitumia kwa Baali.
9Kwa hiyo nitachukua nafaka yake wakati wa mavuno, na divai yangu mpya katika msimu wake. Nitachukua sufu yangu na kitambaa kilichotumiwa kufunika uchi wake.
10Ndipo nitamvua nguo machoni pa wapenzi wake, wala hakuna mtu atakayemwokoa mkononi mwangu.
11Nitasitisha furaha yake yote- sikukuu zake, mwandamo wa mwezi, sabato zake na sikukuu zake zote zilizowekwa.
12Nitaharibu mizabibu yake na mtini wake, ambayo alisema, 'Hii ni mishahara ambayo wapenzi wangu walinipa.' Nitawafanya kuwa msitu, na wanyama wa shambani watakula.
13Nami nitamuadhibu kwa ajili ya Sikukuu ya Baali, alipowafukizia uvumba, akijipamba kwa pete zake na mavazi yake, naye akafuata wapenzi wake, akanisahau.” Hili ndilo tamko la Bwana.
14Kwa hiyo nitaenda kumshawishi. Nitamleta jangwani na kumwambia kwa huruma.
15Nami nitamrudishia mizabibu yake, na bonde la Akori kama mlango wa tumaini. Yeye atanijibu huko kama alivyofanya katika siku za ujana wake, kama katika siku ambazo alitoka katika nchi ya Misri.
16“Itakuwa katika siku hiyo”-hili ndilo tamko la Bwana-”kwamba utaniita, 'Mume wangu,' na hutaniita tena mimi, 'Baal wangu.'
17Kwa maana nitaondoa majina ya Baali kinywani mwake; majina yao hayatakumbukwa tena.”
18“Siku hiyo nitafanya agano pamoja na wanyama katika mashamba kwa ajili yao, na ndege wa angani, na vitu vya kutambaa chini. Nitaondoa upinde, upanga, na vita katika nchi, nami nitakufanya ulale kwa usalama.
19Nitakuwa mume wako milele. Nitakuwa mume wako katika haki, hukumu, uaminifu wa agano, na huruma.
20Nitakuwa mume wako kwa uaminifu. Nawe utanijua mimi, Bwana.
21Na siku ile, nitajibu”-hili ndilo tamko la Bwana. “Nitazijibu mbingu, nao watajibu dunia.
22Dunia itashughulikia nafaka, divai mpya na mafuta, na watajibu Yezreeli.
23Nitatampanda mwenyewe katika nchi kwa ajili yangu, na nitamhurumia Lo Ruhama. Nami nitamwambia Lo Ami, 'Wewe ni Ami Ata,' nao wataniambia, 'Wewe ni Mungu wangu.'”