1Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi.
2Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe.
4Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu.
5Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu,
6kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu,
7udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu.
8Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani.
10Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe.
11Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
12Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea.
13Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya.
14Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi.