1 Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi.
2 Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe.
4 Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu.
5 Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu,
6 kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu,
7 udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu.
8 Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe.
11 Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
12 Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea.
13 Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya.
14 Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi.