10Wala msinung'unike kama baadhi yao walivyonung'unika, wakaangamizwa na Mwangamizi!
11Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi, ambao mwisho wa nyakati unatukabili.
12Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke.
13Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
14Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu.
15Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo.
16Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo?
17Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.
18Chukueni, kwa mfano, Wayahudi wenyewe: kwao, wenye kula vilivyotambikiwa madhabahuni waliungana na hiyo madhabahu.
19Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu?
20Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe ninyi muwe na ushirika na pepo.
21Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika meza ya Bwana na katika meza ya pepo.
22Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye?
23Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga.
24Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake.
25Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu;
26maana Maandiko yasema: “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”
27Kama mtu ambaye si muumini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu.