Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 9

Matendo 9:1-19

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa Kuhani Mkuu,
2akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia ya Bwana, awakamate na kuwaleta Yerusalemu.
3Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote.
4Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: “Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?”
5Naye Saulo akauliza, “Ni nani wewe Bwana?” Na ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.
6Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya.”
7Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu.
8Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko.
9Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote.
10Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, “Anania!” Anania akaitika, “Niko hapa, Bwana.”
11Naye Bwana akamwambia, “Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali;
12na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena.”
13Lakini Anania akajibu, “Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu.
14Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako.”
15Lakini Bwana akamwambia, “Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli.
16Mimi mwenyewe nitamwonyesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu.”
17Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, “Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu.”
18Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa.
19Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko.

Read Matendo 9Matendo 9
Compare Matendo 9:1-19Matendo 9:1-19