Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 7

Luka 7:11-43

Help us?
Click on verse(s) to share them!
11Baadaye kidogo Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake pamoja na kundi kubwa la watu waliandamana naye.
12Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya kijana mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama.
13Bwana alipomwona mama huyo, alimwonea huruma, akamwambia, “Usilie.”
14Kisha akaenda, akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wanalichukua wakasimama. Halafu akasema, “Kijana! Nakuamuru, amka!”
15Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
16Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema: “Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”
17Habari hizo zikaenea kote katika Uyahudi na katika nchi za jirani.
18Wanafunzi wa Yohane walimpa habari Yohane juu ya mambo hayo yote. Naye Yohane, baada ya kuwaita wawili kati ya wanafunzi wake,
19aliwatuma kwa Bwana wamwulize: “Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”
20Wale wanafunzi walipomfikia Yesu wakamwambia, “Yohane Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: Wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”
21Wakati huohuo, Yesu alikuwa anawaponya watu wengi waliokuwa wanateseka kwa magonjwa na waliopagawa na pepo wabaya, akawawezesha vipofu wengi kuona tena.
22Basi, Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane yale mliyojionea na kuyasikia: vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari njema.
23Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami!”
24Hapo wajumbe wa Yohane walipokwisha kwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu juu ya Yohane: “Mlikwenda kule jangwani, hivi mlitaka kuona kitu gani? Mlitaka kuona unyasi unaotikiswa na upepo?
25Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevalia mavazi maridadi? La hasha! Wanaovaa mavazi maridadi na kuishi maisha ya anasa, hukaa katika majumba ya wafalme!
26Basi, niambieni, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
27Huyu Yohane ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: Hapa ni mtumishi wangu, asema Bwana; ninamtuma akutangulie, akutayarishie njia.”
28Yesu akamalizia kwa kusema, “Nawaambieni, kati ya binadamu wote hakuna aliye mkubwa zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa Mungu ni mkubwa zaidi kuliko yeye.”
29Waliposikia hayo watu wote na watoza ushuru waliusifu wema wa Mungu; hao ndio wale waliokuwa wameupokea ubatizo wa Yohane.
30Lakini Mafarisayo na walimu wa Sheria walikataa mpango wa Mungu uliowahusu wakakataa kubatizwa na Yohane.
31Yesu akaendelea kusema, “Basi, nitawafananisha watu wa kizazi hiki na kitu gani? Ni watu wa namna gani?
32Ni kama vijana waliokuwa wamekaa sokoni na kuambiana, kikundi kimoja na kingine: Tumewapigieni ngoma, lakini hamkucheza! Tumeomboleza, lakini hamkulia!
33Kwa maana Yohane alikuja, yeye alifunga na hakunywa divai, nanyi mkasema: Amepagawa na pepo!
34Akaja Mwana wa Mtu; anakula na kunywa, mkasema: Mwangalieni mlafi huyu na mlevi; rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi!
35Hata hivyo, hekima ya Mungu imethibitishwa kuwa njema na wote wale wanaoikubali.”
36Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani mwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula.
37Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa anaishi maisha mabaya. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.
38Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi.
39Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, “Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.”
40Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, “Simoni, ninacho kitu cha kukwambia.” Naye Simoni akamwambia, “Ndio Mwalimu, sema.” Yesu akasema,
41“Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: mmoja alikuwa amekopa dinari mia tano, na mwingine hamsini.
42Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?”
43Simoni akamjibu, “Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana.” Yesu akamwambia, “Sawa.”

Read Luka 7Luka 7
Compare Luka 7:11-43Luka 7:11-43