Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 2 Wakorintho

2 Wakorintho 1

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, na kwa waumini wote walioko katika mkoa wote wa Akaya.
2Neema na iwe kwenu na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3Na asifiwe Mungu na Baba wa Bwana Yesu Kristo. Yeye ni Baba wa rehema na Mungu wa faraja yote.
4Mungu hutufariji sisi katika mateso yetu yote, ili kwamba tuweze kuwafariji wale walio katika mateso. Tunawafariji wengine kwa faraja ileile ambayo Mungu alitumia kutufariji sisi.
5Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo huongezeka kwa ajili yetu, vile vile faraja yetu huongezeka kupitia Kristo.
6Lakini kama tunataabishwa, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na kama tunafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu. Faraja yenu inafanya kazi kikamilifu mnaposhiriki mateso kwa uvumilivu kama sisi pia tunavyoteseka.
7Na ujasiri wetu juu yenu ni thabiti. Tunajua kwamba kama vile ambavyo mnashiriki mateso, vile vile mnashiriki faraja.
8Kwa kuwa hatutaki ninyi muwe wajinga, ndugu, kuhusu matatizo tuliyokuwa nayo huko Asia. Tulionewa zaidi ya vile tuwezavyo kubeba, kana kwamba hatukuwa hata na tumaini la kuishi tena.
9Kweli, tulikuwa na hukumu ya kifo juu yetu. Lakini hiyo ilikuwa ni kutufanya sisi tusiweke tumaini juu yetu wenyewe, badala yake tuweke tumaini katika Mungu, afufuaye wafu.
10Alituokoa sisi kutoka hayo maafa ya mauti, na atatuokoa tena. Tumeweka ujasiri wetu katika yeye ya kwamba atatuokoa tena.
11Atafanya hivi kama vile ninyi pia mtusaidiavyo kwa maombi yenu. Hivyo wengi watatoa shukurani kwa niaba yetu kwa ajili ya upendeleo wa neema tuliyopewa sisi kupitia maombi ya wengi.
12Tunajivunia hili: ushuhuda wa dhamiri yetu. Kwa kuwa ni katika nia safi na usafi wa Mungu kwamba tulienenda wenyewe katika dunia. Tumefanya hivi hasa na ninyi, na sio katika hekima ya ulimwengu, lakini badala yake ni katika neema ya Mungu.
13Hatuwaandikii chochote ambacho hamwezi kukisoma au kuelewa. Ninaujasiri
14kwamba kwa sehemu mumekwisha kutuelewa. Na ninaujasiri kwamba katika siku ya Bwana Yesu tutakuwa sababu yenu kwa ajili ya kiburi chenu, kama vile mtakavyokuwa kwetu.
15Kwa sababu nilikuwa na ujasiri kuhusu hili, nilitaka kuja kwenu kwanza, ili kwamba muweze kupokea faida ya kutembelewa mara mbili.
16Nilikuwa napanga kuwatembelea wakati nikielekea Makedonia. Tena nilitaka kuwatembelea tena wakati nikirudi kutoka Makedonia, na kisha ninyi kunituma mimi wakati nikielekea Uyahudi.
17Nilipokuwa nafikiria namna hii, je, nilikuwa nasitasita? Je ninapanga mambo kulingana na viwango vya kibinadamu, ili kwamba niseme “Ndiyo, ndiyo” na “Hapana, hapana” kwa wakati mmoja?
18Lakini kama vile Mungu alivyo mwaminifu, hatusemi vyote “Ndiyo” na “Hapana.”

19Kwa kuwa mwana wa Mungu, Yesu Kristo, ambaye Silvano, Timotheo na mimi tulimtangaza miongoni mwenu, siyo “Ndiyo” na “Hapana.” Badala yake, yeye wakati wote ni “Ndiyo.”
20Kwa kuwa ahadi zote za Mungu ni “Ndiyo” katika yeye. Hivyo pia kupitia yeye tunasema “Amina” kwa utukufu wa Mungu.
21Sasa ni Mungu ambaye hututhibitisha sisi pamoja nanyi katika Kristo, na alitutuma sisi.
22Aliweka muhuri juu yetu na alitupa Roho katika mioyo yetu kama dhamana ya kile ambacho angetupatia baadaye.
23Badala yake, namsihi Mungu kunishuhudia mimi kwamba sababu iliyonifanya nisije Korintho ni kwamba nisiwalemee ninyi.
24Hii sio kwa sababu tunajaribu kudhibiti jinsi imani yenu inavyotakiwa kuwa. Badala yake, tunafanya pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu, kama mnavyosimama katika imani yenu.