1Hivyo, mtu mmoja aliyeitwa Anania, na Safira mkewe, waliuza sehemu ya mali,
2na akaficha sehemu ya fedha waliyouza (mke wake pia alilijua hili), na akaleta sehemu iliyobakia na kuiweka kwenye miguu ya mitume.
3Lakini Petro akasema, “Anania, kwa nini shetani ameujaza moyo wako kusema uongo kwa Roho Mtakatifu na kuficha sehemu ya mali ya shamba?
4Wakati lilipokuwa halijauzwa, halikuwa ni mali yako? Na baada ya kuuzwa, halikuwa chini ya uamuzi wako? Ilikuwaje uwaze jambo hili moyoni mwako? Hujawadanganya wanadamu, bali umemdanganya Mungu.”
5Katika kusikia maneno haya, Anania alidondoka chini na akakata roho. Na hofu kubwa iliwajia wote waliolisikia hili.
6Vijana wakaja mbele na kumtia katika sanda, na kumpeleka nje na kumzika.
7Baada ya masaa matatu hivi, mke wake aliingia ndani, asijue ni nini kilichokuwa kimetokea.
8Petro akamwambia, “Niambie, kama mliuza shamba kwa thamani hiyo.” Akasema, “Ndiyo, kwa thamani hiyo.”
9Kisha Petro akamwambia, “Inakuwaje kwamba mmepatana kwa pamoja kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu ya wale waliomzika mme wako iko mlangoni, na watakubeba na kukupeleka nje.”
10Ghafla akadondoka miguuni pa Petro, akakata roho, na wale vijana wakaja ndani wakamkuta ameshakufa. Wakambeba kumpeleka nje, na kumzika karibu na mmewe.
11Hofu kubwa ikaja juu ya kanisa zima, na juu ya wote walioyasikia mambo haya.
12Ishara nyingi na maajabu vilikuwa vinatokea miongoni mwa watu kupitia mikono ya mitume. Walikuwa pamoja katika ukumbi wa Sulemani.
13Lakini, hakuna mtu mwingine tofauti aliyekuwa na ujasiri wa kuambatana nao; hata hivyo, walipewa heshima ya juu na watu.
14Na pia, waamini wengi walikuwa wakiongezeka kwa Bwana, idadi kubwa ya wanaume na wanawake,
15kiasi kwamba hata waliwabeba wagonjwa mitaani, na kuwalaza vitandani na kwenye makochi, ili kwamba Petro akiwa anapita, kivuli chake kiweze kushuka juu yao.
16Hapo pia, idadi kubwa ya watu walikuja kutoka miji iliyozunguka Yerusalem, wakiwaleta wagonjwa na wote waliopagawa na roho wachafu, na wote waliponywa.
17Lakini kuhani mkuu aliinuka, na wote waliokuwa pamoja naye (ambao ni wa dhehebu la masadukayo); na walijawa na wivu
18wakanyosha mikono yao kuwakamata mitume na kuwaweka ndani ya gereza la jumla.
19Na wakati wa usiku malaika wa Bwana akaifungua milango ya gereza na kuwaongoza nje na kusema,
20“Nendeni, mkasimame hekaluni na kuwaambia watu maneno yote ya Uzima huu.”
21Waliposikia hili, waliingia hekaluni wakati wa kupambazuka na kufundisha. Lakini, kuhani mkuu alikuja na wote waliokuwa naye, na kuitisha baraza lote kwa pamoja, na wazee wote wa watu wa Israeli, na kuwatuma gerezani ili kuwaleta mitume.
22Lakini watumishi waliokwenda, hawakuwakuta gerezani, walirudi na kutoa taarifa,
23“Tumekuta gereza limefungwa vizuri salama, na walinzi wamesimama langoni, lakini tulipokuwa tukifungua, hatukuona mtu ndani.”
24Sasa wakati jemedari wa hekalu na makuhani wakuu waliposikia maneno haya, waliingiwa na shaka kubwa kwa ajili yao wakiwaza litakuwaje jambo hili.
25Kisha mmoja akaja na kuwaambia, “Watu mliowaweka gerezani wamesimama hekaluni na wanafundisha watu.”
26Hivyo jemedari alienda pamoja na watumishi, na wakawaleta, lakini bila ya kufanya vurugu, kwa sababu waliwaogopa watu wangeweza kuwapiga kwa mawe.
27Walipokwisha kuwaleta, waliwaweka mbele ya baraza. Kuhani mkuu aliwahoji
28akisema, “Tuliwaamuru msifundishe kwa jina hili, na bado mmeijaza Yerusalemu kwa fundisho lenu, na kutamani kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
29Lakini Petro na mitume wakajibu, “Lazima tumtii Mungu kuliko watu.
30Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, mliyemuua, kwa kumtundika juu ya mti.
31Mungu alimtukuza katika mkono wake wa kuume, na kumfanya kuwa Mkuu na mwokozi, kutoa toba kwa Israeli, na msamaha wa dhambi.
32Sisi ni mashahidi wa mambo haya, na Roho Mtakatifu, ambaye Mungu amemtoa kwa wale wanaomtii.”
33Wajumbe wa baraza waliposikia hivi, walishikwa na hasira wakataka kuwaua mitume.
34Lakini pharisayo aliyeitwa Gamalieli, mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, alisimama na kuwaamuru mitume wachukuliwe nje kwa muda mfupi.
35Kisha akawaambia, “Wanaume wa Israeli, iweni makini sana na kile mnachopendekeza kuwafanyia watu hawa.
36Kwa sababu, zamani zilizopita, Theuda aliinuka na kujidai kuwa mtu mkuu, na idadi ya watu, wapata mia nne walimfuata. Aliuawa, na wote waliokuwa wanamtii walitawanyika na kupotea.
37Baada ya mtu huyu, Yuda mgalilaya, aliinuka siku zile za kuandikwa sensa, akavuta watu wengi nyuma yake. Naye pia alipotea na wote waliokuwa wakimtii walitawanyika.
38Sasa nawaambia, jiepusheni na watu hawa na muwaache wenyewe, kwa sababu, kama mpango huu au kazi hii ni ya watu itatupwa.
39Lakini kama ni ya Mungu, hamtaweza kuwazuia; mnaweza mkajikuta hata mnashindana na Mungu.” Hivyo, walishawishika na maneno yake.
40Kisha, waliwaita mitume ndani na kuwachapa na kuwaamuru wasinene kwa jina la Yesu, na wakawaacha waende zao.
41Waliondoka mbele ya baraza wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuteseka na kutoheshimiwa kwa ajili ya Jina hilo.
42Kwa hiyo, kila siku, ndani ya hekalu na kutoka nyumba hadi nyumba waliendelea kufundisha na kuhubiri Yesu kuwa ni Masihi.