Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Matendo ya Mitume

Matendo ya Mitume 22

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1“Ndugu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu nitakaofanya kwenu sasa.”
2Makutano walipo sikia Paulo akiongea nao kwa kiebrania, wakanyamaza. Akasema,
3“Mimi ni myahudi, nimezaliwa mji wa Tarso eneo la Kilikia, ila nilipata elimu katika mji huu, miguuni pa Gamalieli. Nilifundishwa kulingana na njia sahihi za sheria za baba zetu. Mimi ninabidii ya Mungu, kama ninyi nyote mlivyo leo.
4Niliwatesa kwa njia hii hadi kufa; nikawafunga wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.
5Hata kuhani mkuu na wazee wote wanaweza kutoa ushahidi kwamba nilipokea barua kutoka kwao kwa ajili ya ndugu walio Dameski, kwangu mimi kusafiri kwenda huko. Ilikuwa niwalete watu Yerusalemu wa njia ile ili wafungwe na kuadhibiwa.
6Ilitokea kwamba pale nilipokua nikisafiri nakaribia Dameski, majira ya mchana ghafla nuru kuu ikatokea mbinguni ikaanza kuniangaza.
7Nikaanguka chini na kusikia sauti ikiniambia, 'Sauli, Sauli kwanini unaniudhi?'
8Nikajibu, 'wewe ni nani, Bwana?' Akaniambia, 'Mini ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.'
9Wale waliokuwa na mimi waliiona nuru, ila hawakusikia sauti ya yule alie ongea na mimi.
10Nikasema, 'Nifanye nini, Bwana?' Bwana akaniambia, 'Simama na uingie Dameski; huko utaambiwa kila kitu unachopaswa kufanya.'
11Sikuweza kuona kwa sababu ya muangaza wa nuru ile, ndipo nikaenda Dameski kwa kuongozwa na mikono ya wale waliokuwa na mimi.
12Huko nikakutana na mtu aitwaye Anania, alikuwa mtu aliyeshika sheria na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote walioishi huko.
13Akaja kwangu, akasimama mbele yangu, na kusema, 'Ndugu yangu Sauli, upate kuona.' Kwa muda ule ule nikamuona.
14Akasema, 'Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, kumuona yule mwenyehaki, na kusikia sauti itokayo kwenye kinywa chake.
15Kwa sababu utakuwa shahidi kwake kwa watu wote juu ya uliyoyaona na kusikia.
16Basi sasa kwa nini unasubiri? Amka, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliita jina lake.'
17Baada ya kurejea Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, ikatokea kwamba nikapewa maono.
18Nikamuona akiniambia, 'Hima na utoke Yerusalemu haraka, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu mimi.'

19Nikasema, 'Bwana, wao wenyewe wanajua niliwafunga gerezani na kuwapiga wale waliokuamini katika kila sinagogi.
20Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, Mimi pia nilikuwa nimesimama karibu na kukubali na nilikuwa nalinda nguo za wale waliomwua.'
21Lakini aliniambia, 'Enenda, kwa sababu mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa mataifa.”'
22Watu wakamruhusu aongee juu ya neno hili. Lakini baadaye walipaza sauti na kusema, “mwondoe mtu huyu katika nchi: kwa sababu sio sahihi aishi.”
23Walipokuwa wakipaza sauti, na kutupa mavazi yao na kutupa mavumbi juu,
24jemedari mkuu akaamuru Paulo aletwe ngomeni. Akaamuru aulizwe huku anapigwa mijeledi, ili yeye mwenyewe ajue kwa nini walikuwa wanampigia kelele namna ile.
25Hata walipokuwa wamemfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliye simama karibu naye, “Je! ni haki kwenu kumpiga mtu aliye Mrumi na bado hajahukumiwa?”
26Yule akida aliposikia maneno haya, akaenda kwa jemedari mkuu na kumwambia, akisema, “Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni mrumi.”
27Jemedari mkuu akaja na kumwambia, “Niambie, je wewe ni raia wa Rumi?” Paulo akasema, “Ndiyo.”
28Jemedari akamjibu, “Ni kupitia kiasi kikubwa cha pesa ndipo nilipata uraia.” Lakini Paulo akamwambia, “Mimi ni mrumi wa kuzaliwa.”
29Basi wale waliokuwa tayari kwenda kumuuliza wakaondoka na kumwacha wakati huo huo. Na jemedari naye akaogopa, alipojua kuwa Paulo ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga.
30Siku iliyofuatayo, jemedari mkuu alitaka kujua ukweli kuhusu mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Paulo. Hivyo akamfungua vifungo vyake akaamuru wakuu wa makuhani na baraza lote wakutane. Akamleta Paulo chini, na kumweka katikati yao.