1Na walipopita katika miji ya Amfipoli na Apolonia, walikuja mpaka mji wa Thesalonike ambao kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2Kama ilivyo kawaida ya Paulo, alienda kwao, na kwa muda wa siku tatu za Sabato alijadiliana nao juu ya maandiko.
3Alikuwa akiwafungulia maandiko na kuwaeleza kuwa, ilimpasa Kristo ateseke na kisha kufufuka tena kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Kristo”
4Baadhi ya Wayahudi walishawishika na kuungana na Paulo na Sila, pamoja na Wagiriki wachamungu, akinamama wengi waongofu na kundi kubwa la watu.
5Lakini baadhi ya Wayahudi wasioamini, waliojawa na wivu, walienda sokoni na kuwachukuwa baadhi ya watu waovu, wakakusanya umati wa watu pamoja, na kusababisha ghasia mjini, kisha wakaivamia nyumba ya Jason, wakitaka kuwakamata Paulo na Sila ilikuwaleta mbele za watu.
6Lakini walipowakosa, walimkamata Yasoni na baadhi ya ndugu wengine na kuwapeleka mbele ya maofisa wa mji, wakipiga kelele, “Hawa wanaume walioupindua ulimwengu wamefika mpaka huku pia,
7Wanaume hawa waliokaribishwa na Yasoni wanaihalifu sheria ya Kaisari, wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu”
8Umati na maofisa wa mji waliposikia mambo hayo, waliingiwa na wasiwasi.
9Baada ya kuwa wamekwisha kuchukua fedha ya thamani ya ulinzi kutoka kwa Yason na wengine, waliwaachia waende.
10Usiku ule ndugu walimtuma Paulo na Sila Beroya. Na walipofika kule walikwenda katika sinagogi la Wayahudi.
11Watu wale walikuwa wenye werevu mkubwa kuliko wale watu wa Thesalonike, kwa sababu walikuwa na utayari wa kulipokea neno kwa akili zao, na kuchunguza maandiko kila siku ili kuona kama maneno yaliyonenwa ndivyo yalivyo.
12Kwa hiyo wengi wao waliamini, wakiwemo wanawake wenye ushawishi mkubwa wa Kigiriki na wanaume wengi.
13Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo anatangaza neno la Mungu huko Beroya, walienda huko na kuchochea na kisha kuanzisha ghasia kwa watu.
14Kwa haraka, ndugu wakampeleka Paulo kwa njia ya ziwa, lakini Sila na Timotheo wakabaki pale.
15Wale ndugu waliompeleka Paulo walienda naye hadi Athene, walipomwacha Paulo huko, walipokea maagizo kutoka kwake kuwa, Sila na Timotheo waje kwake kwa haraka iwezeanavyo.
16Na wakati akiwasubiri huko Athene, roho yake ilikasirishwa ndani yake kwa jinsi alivyouona mji ulivyojaa sanamu nyingi.
17Hivyo akajadiliana katika sinagogi na wayahudi wale waliomcha Mungu na kwa wale wote aliokutana nao kila siku sokoni.
18Lakini baathi ya Wanafalsafa wa Waepikureo na Wastoiko wakamkabili. Na wengine wakasema, “Ni nini anachokisema huyu mwongeaji mchanga? Wengine wakasema, “inaonekana anahubiri habari ya mungu mgeni,” kwasababu anahubiri habari ya Yesu na ufufuo.
19Wakamchukua Paulo na kumleta Areopago, wakisema, “Twaweza kujua haya mafundisho mapya unayoyaongea?
20Kwasababu unaleta mambo mapya katika masikio yetu. Kwahivyo tunataka kujua haya mambo yana maana gani?”
21(Na watu wote wa Athene pamoja na wageni waliopo kwao, hutumia muda wao aidha katika kuongea na kusikiliza juu ya jambo jipya.)
22Kwa hiyo Paulo akasimama katikati ya watu wa Areopago na kusema, “Enyi watu wa Athene, naona kuwa ninyi ni watu wa dini kwa kila namna,
23Kwani katika kupita kwangu na kuangalia vitu vyenu vya kuabudu, nimeona maneno yalioandikwa kwenye moja ya madhabahu yenu, ikisema “KWA MUNGU ASIYEJULIKANA”. Hivyo basi, huyo mnayemwabudu pasipokujua, ndiye ninayewajulisha ninyi.
24Mungu aliyeumba dunia na kila kitu kilichoko ndani, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hawezi kukaa katika mahekalu yaliyotengenezwa na mikono.
25Na pia hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu kwao, kwani yeye mwenyewe huwapa watu uzima na pumzi na vitu vingine vyote.
26Kupitia mtu mmoja, alifanya mataifa yote ya watu waishio juu ya uso wa dunia, na akawawekea nyakati na mipaka katika maeneo wanaoishi.
27Kwa hiyo, wanatakiwa kumtafuta Mungu, na yamkini wamfikie na kumpata, na kwa uhakika hayupo mbali na kila mmoja wetu.
28Kwake tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu, kama vile mtunzi wenu mmoja wa shairi aliposema 'tu wazaliwa wake.'
29Kwa hiyo, ikiwa sisi ni wazaliwa wa Mungu, hatupaswi kufikiri kuwa uungu ni kama dhahabu, au shaba, au mawe, sanamu iliyochongwa kwa ustadi na mawazo ya watu.
30Kwa hiyo, Mungu alinyamazia nyakati zile za ujinga, lakini sasa anaamuru watu wote kila mahali wapate kutubu.
31Hii ni kwa sababu ameweka siku atakayo ihukumu dunia kwa haki kwa mtu ambaye alimchagua. Mungu alitoa uhakika wa mtu huyu kwa kila mtu pale alipomfufua katoka kwa wafu.
32Na watu wa Athene waliposikia habari ya kufufuliwa kwa wafu, baadhi yao wakamdhihaki Paulo, ila wengine wakasema “Tutakusikiliza tena kwa habari ya jambo hili”
33Baada ya hapo, Paulo akawaacha.
34Lakini baadhi ya watu waliungana naye wakaamini, akiwemo Dionisio Mwareopago, na Mwanamke anaitwa Damari na wengine pamoja nao.