22Ndipo binti wa Herodia akaingia na kucheza mbele yao, akamfurahisha Herode na wageni walioketi wakati wa chakula cha jioni. Ndipo mfalme akamwambia binti, “Niombe chochote unachotaka nami nitakupa.”
23Akamwapia na kusema, chochote utakachoniomba, nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.”
24Akatoka nje akamuuliza mama yake, “Niombe nini?” Akasema, “Kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
25Na mara moja akaingia kwa mfalme akaanza kusema, “Nataka unipatie ndani ya sahani, kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
26Mfalme alisikitishwa sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake na kwa ajili ya wageni, hakuweza kumkatalia ombi lake.
27Hivyo, mfalme akatuma askari kati ya walinzi wake na kuwaagiza kwenda kumletea kichwa cha Yohana. Mlinzi alikwenda kumkata kichwa akiwa kifungoni.
28Akakileta kichwa chake kwenye sahani na kumpatia binti, na binti akampa mama yake.
29Na wanafunzi wake waliposikia hayo, walikwenda kuuchukua mwili wake wakaenda kuuzika kaburini.
30Na mitume, walikusanyika pamoja mbele ya Yesu, wakamweleza yote waliyofanya na waliyoyafundisha.
31Naye akawaambia, “Njooni wenyewe mahali pa faragha na tupumzike kwa muda.” Watu wengi walikuwa wanakuja na kuondoka, hata hawakupata nafasi ya kula.
32Hivyo wakapanda mashua wakaenda mahali pa faragha peke yao.
33Lakini waliwaona wakiondoka na wengi wakawatambua, kwa pamoja walikimbia kwa miguu kutoka miji yote, nao wakafika kabla yao.
34Walipofika pwani, aliona umati mkubwa na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Na akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35Muda ulipoendelea sana, wanafunzi wakamjia wakamwambia, “Hapa ni mahali pa faragha na muda umeendelea.
36Uwaage waende miji ya jirani na vijiji ili wakajinunulie chakula.”
37Lakini akawajibu akisema, “Wapeni ninyi chakula.” Wakamwambia, “Tunaweza kwenda na kununua mikate yenye thamani ya dinari mia mbili na kuwapa wale?”