24akaniambia: Paulo usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.
25Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa.
26Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani.”
27Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huku katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu.
28Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arobaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini.
29Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi.
30Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli.
31Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, “Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka.”
32Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji.
33Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula: “Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala kitu chochote.
34Basi, ninawasihi mle chakula kwa maana mnakihitaji ili mweze kuendelea kuishi. Maana hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.”
35Baada ya kusema hivyo, Paulo alichukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula.
36Hapo wote wakapata moyo, nao pia wakala chakula.
37Jumla tulikuwa watu mia mbili na sabini na sita katika meli.
38Baada ya kila mmoja kula chakula cha kutosha, walipunguza uzito wa meli kwa kutupa nafaka baharini.
39Kulipokucha, wanamaji hawakuweza kuitambua nchi ile, ila waliona ghuba moja yenye ufuko; wakaamua kutia nanga huko kama ikiwezekana.