Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 9

Luka 9:21-50

Help us?
Click on verse(s) to share them!
21Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo.
22Akaendelea kusema: “Ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria; atauawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa.”
23Kisha akawaambia watu wote, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.
24Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa.
25Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe?
26Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.
27Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu.”
28Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali.
29Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kung'aa sana.
30Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao ni Mose na Eliya,
31ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kifo chake ambacho angekikamilisha huko Yerusalemu.
32Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.
33Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri kwamba tupo hapa: basi, tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya.” —Kwa kweli hakujua anasema nini.
34Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana.
35Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: “Huyu ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni.”
36Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona.
37Kesho yake walipokuwa wakishuka kutoka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu.
38Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaaza sauti, akasema, “Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu—mwanangu wa pekee!
39Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele; humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache upesi.
40Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza.”
41Yesu akasema, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?” Kisha akamwambia huyo mtu, “Mlete mtoto wako hapa.”
42Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake.
43Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu. Wale watu walipokuwa bado wanashangaa juu ya mambo yote aliyofanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake,
44“Tegeni masikio, myasikie mambo haya: Mwana wa Mtu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu.”
45Lakini wao hawakuelewa maana ya usemi huo. Jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao ili wasitambue; nao wakaogopa kumwuliza juu ya msemo huo.
46Kukatokea majadiliano kati ya wale wanafunzi kuhusu nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi.
47Yesu aliyajua mawazo yaliyokuwa mioyoni mwao; basi akamchukua mtoto mdogo akamweka karibu naye,
48akawaambia, “Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkubwa kuliko wote.”
49Yohane alidakia na kusema, “Bwana, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.”
50Lakini Yesu akamwambia, “Msimkataze; kwani asiyepingana nanyi yuko upande wenu.”

Read Luka 9Luka 9
Compare Luka 9:21-50Luka 9:21-50