Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Danieli

Danieli 6

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Ilimpendeza Dario kuchagua juu ya ufalme magavana wa majimbo 120 ambao wangetawala juu ya ufalme wote.
2Juu yao kulikuwa na watawala wakuu watatu, na Daniel alikuwa mmoja wao. Hawa watawala waliwekwa ili waweze kuwasimamia magavana wa majimbo, ili kwamba mfalme asipate hasara.
3Danieli alipambanuliwa juu ya watawala wakuu na juu ya magavana wa majimbo kwasababu alikuwa na roho isiyo ya kawaida. Mfalme alikuwa akipanga kumweka juu ya ufalme wote.
4Basi watawala wakuu wengine na magavana wa majimbo walitafuta makosa katika kazi ambazo Danieli alizifanya kwa ufalme, lakini hawakuweza kuona ufisadi au kushindwa katika majukumu yake kwasababu alikuwa mwaminifu. Hakuna kosa au uzembe uliopatikana ndani yake.
5Kisha watu hawa wakasema, “Hatukuweza kupata sababu yoyote ya kumshitaki huyu Danieli isipokuwa tukitafuta kitu fulani dhidi yake kuhusiana na sheria za Mungu wake.'”
6Ndipo watawala hawa na magavana walileta mpango mbele ya mfalme. Walimwambia, “Mfalme Dario, uishi milele!
7Watawala wote wakuu wa ufalme, magavana wa mikoa, na magavana wa majimbo, washauri, na magavana wameshauriana kwa pamoja na kuamua kuwa wewe, mfalme, unapaswa kupitisha amri na kuitekeleza, ili kwamba mtu yeyote anayefanya dua kwa mungu yeyote au mtu kwa siku thelathini, isipokuwa wewe mfalme, mtu huyo lazima atupwe katika tundu la simba.
8Sasa mfalme, litoe agizo na utie saini nyaraka ili kwamba isije ikabadilika, kama ilivyoelekezwa katika sheria za Wamedi na Waajemi, hivyo haiweze ikabatilishwa.
9Basi, mfalme Dario alitia saini nyaraka kwa kuifanya amri kuwa sheria.
10Danieli alipojua kuwa nyaraka imekwisha kusainiwa kuwa sheria, alienda ndani ya nyumba yake (madirisha yake katika chumba cha juu yalikuwa wazi kuelekea Yerusalemu), na alipiga magoti yake, kama alivyokuwa akifanya mara tatu kwa siku, na aliomba na kushukuru mbele ya Mungu wake, kama alivyofanya hapo kabla.
11Kisha watu hawa walikuwa wameunda hila kwa pamoja walimwona Danieli akiomba na kutafuta msaada kutoka kwa Mungu.
12Ndipo walipomwendea mfalme na kuongea naye kuhusiana na amri yake: “Je haukuweka amri kwamba mtu yeyote akayefanya maombi kwa mungu mwingine au kwa binadamu ndani ya siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, mfalme, lazima mtu huyo atupwe katika tundu la simba? Mfalme akajibu, “Jambo hili ni la hakika, kama ilivyoelekezwa katika sheria za Wamedi na Waajemi; ambazo haziwezi zikabatilishwa.”
13Kisha wakamjibu mfalme, “Mtu yule Daniel, ambaye ni mmoja wa watu wa mateka kutoka Yuda, hakutii wewe, mfalme wala maagizo yako uliyoyasaini. Yeye humwomba Mungu wake mara tatu kwa siku.”
14Mfalme aliposikia haya, alisikitishwa sana, alitumia akili jinsi ya kumwokoa kutoka katika utawala huu. Alisumbuka sana mpaka wakati wa kuzama kwa jua akijaribu kumwokoa Danieli.
15Kisha watu hawa waliokuwa wamepanga njama walikusanyika kwa pamoja na mfalme, na wakamwambia, “Ujue mfalme kwamba ni sheria ya Wamedi na Waajemi kwamba hakuna amri au sanamu ambayo mfalme anaipitisha yaweza kubadilishwa.”
16Ndipo mfalme alitoa agizo, na walimleta ndani Danieli, na kisha wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako, ambaye unamtumikia daima, na akuokoe.''
17Jiwe lililetwa katika mlango wa tundu, na mfalme alilitia muhuri wa pete yake mwenyewe na pamoja na muhuri wa wakuu wake ili kwamba chochote kisiweze kubadilishwa kuhusiana na Danieli.
18Basi mfalme alienda kwenye ikulu yake na usiku ule alikuwa na mfungo. Hakuna starehe yoyote iliyoletwa mbele yake, nao usingizi ulimkimbia.

19Kisha katika mapambazuko mfalme aliamka na kwa haraka alienda kwenye tundu la simba.
20Na alipokaribia kwenye tundu, alimwita Danieli kwa sauti ya huzuni, akimwambia Danieli, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je Mungu wako ambaye anamtumkia daima ameweza kukuokoa kutoka katika simba?
21Ndipo Danieli akamwambia mfalme, “Mfalme, uishi milele!
22Mungu wangu amemtuma mjumbe na amevifunga vinywa vya simba, na hazijaweza kunidhuru. Kwa kuwa sikuwa na hatia yoyote mbele yake na pia mbele yako, ewe mfalme, na sijakufanyia jambo lolote la kukudhuru.”
23Basi mfalme alikuwa na furaha sana. Alitoa agizo kwamba wanatakiwa wamtoe Danieli nje ya tundu. Hivyo Danieli aliondolewa kutoka katika tundu. Hakuna dhara lolote lililoonekana kwake, kwa kuwa alikuwa amemtumainia Mungu wake.
24Mfalme alitoa agizo, waletwe wale watu waliomshitaki Danieli na kisha akawatupa wao katika tundu la simba - wao, na watoto wao, na wake zao. Kabla hawajafika sakafuni, simba waliwararua na kuvunjavunja mifupa yao vipande vipande.
25Kisha mfalme Dario aliandika ujumbe kwa watu wote, mataifa na lugha ambazo ziliishi katika dunia yote: “Amani na iongezeke kwenu.
26Ninaagiza kwamba katika utawala wote wa ufalme wangu watu watetemeka na kumcha mbele ya Mungu wa Danieli, kwa kuwa ni Mungu aliye hai na huishi milele, na ufalme wake hauwezi kuharibiwa; utawala wake utakuwepo hadi mwisho.
27Yeye anatuhifadhi salama na kutuokoa, na anafanya ishara na maajabu mbinguni na duniani; amemhifadhi Danieli salama dhidi ya uwezo wa simba.”
28Na hivyo basi, Danieli alifanikiwa katika utawala wa Dario na katika utawala wa Koreshi Mwajemi.