Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mathayo

Mathayo 24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Yesu alitoka hekaluni na kwenda zake. Wanafunzi wake walimwendea na kumuonesha majengo ya hekalu.
2Laikni aliwajibu na kuwaambia, “Je, hamuyaoni mambo haya yote? Kweli nawaambia, hakuna jiwe litalobaki juu ya lingine bila kubomolewa.”
3Na alipokaa katika Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake walimwendea kwa faragha na kusema, “Tuambie, mambo haya yatatokea lini? Kitu gani kitakuwa dalili ya kuja kwako na mwisho wa ulimwengu?”
4Yesu aliwajibu na kuwaambia, “Iweni makini kwamba asije mtu akawapotosha.
5Kwa kuwa wengi watakuja kwa jina langu. Watasema, 'Mimi ndiye Kristo', na watawapotosha wengi.
6Mtasikia vita na taarifa za vita. Angalieni msije mkawa na wasiwasi, kwa kuwa mambo haya hayabudi kutokea; lakini ule mwisho utakuwa bado.
7Kwa kuwa taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na matetemeko ya ardhi katika sehemu mbalimbali.
8Lakini mambo haya yote ni mwanzo tu wa uchungu wa kujifungua.
9Ndipo watawatoa kwa ajili ya mateso na kuwaua. Mtachukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina langu.
10Ndipo wengi watajikwaa na kusalitiana na watachukiana wenyewe kwa wenyewe.
11Manabii wengi wa uongo watatokea na kuwadanganya wengi.
12Kwa sababu uovu utaongezeka, upendo wa wengi utapoa.
13Lakini atakaye vumilia mpaka mwisho, ataokolewa.
14Hii Injili ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu mzima kama ushuhuda kwa mataifa yote. Na ndipo ule mwisho utafika.
15Kwa hiyo, mtakapoona chukizo la uharibifu, lililosemwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu asomaye na afahamu,
16ndipo walioko Yuda wakimbilie milimani.
17Na yule aliyeko juu ya paa la nyumba asiweze kuteremka chini kuchukua kitu chochote kutoka ndani ya nyumba yake,
18naye aliyeko shambani asirudi kuchukua vazi lake.

19Lakini ole wao ambao wana mtoto na wale ambao wananyonyesha katika siku hizo!
20Ombeni kwamba kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.
21Kwa kuwa kutakuwa na dhiki kuu, ambayo haijawahi kuwapo tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi sasa, na wala haitakuwapo tena.
22Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna ambaye angeokoka. Lakini kwa sababu ya wateule, siku hizo zitafupishwa.
23Kisha ikiwa mtu yeyote atawaambia 'Tazama, Kristo yuko hapa! au, 'Kristo yuko kule' msiamini maneno hayo.
24Kwa kuwa Makristo wa uongo na manabii wa uongo watakuja na kuonesha ishara kubwa na maajabu, kwa kusudi la kupotosha, kama ingewezekana hata na wateule.
25Tazameni, nimewatahadharisha kabla ya mambo hayo kutokea.
26Kwa hiyo, ikiwa watawaambia, ''Kristo yuko jangwani,' msiende huko jangwani. Au, 'Tazameni, yuko ndani ya nyumba,' msiamini maneno hayo.
27Kama vile radi inavyomulika kutokea mashariki na kuangaza hadi magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu.
28Popote ulipo mzoga, huko ndiko tai wakusanyikapo.
29Lakini mara baada ya dhiki kuu ya siku zile, Jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbinguni zitatikisika.
30Ndipo ishara ya Mwana wa Adamu itaonekana angani, na makabila yote ya dunia wataomboleza. Watamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani kwa nguvu na utukufu mkuu.
31Atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya pamoja wateule wake kutoka pande nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.
32Jifunzeni somo kutokana na mti mtini. Mara tu tawi linapochipuka na kutoa majani, mnajua kwamba kiangazi kinakaribia.
33Hivyo pia, mtakapoona mambo haya yote, mnapaswa kujua kwamba amekaribia, karibu na malango.
34Kweli nawaambia, kizazi hiki hakitapita, hadi mambo yote haya yatakuwa yametokea.
35Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
36Lakini kuhusu siku ile na saa hakuna mtu ajuaye, hata malaika wa mbinguni, wala Mwana, bali Baba peke yake.

37Kama vile ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu.
38Kwa kuwa katika siku hizo kabla ya gharika watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa hadi siku ile ambayo Nuhu aliingia katika safina,
39na hawakujua kitu chochote hadi gharika ilipokuja na kuwasomba wote - ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu.
40Ndipo watu wawili watakuwa shambani- mmoja atachukuliwa, na mmoja ataachwa nyuma.
41Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja - mmoja atachukuliwa, na mmoja atabaki.
42Kwa hiyo, kuweni macho kwa sababu hamjui ni siku gani ambayo atakuja Bwana wenu.
43Lakini mjue kwamba, ikiwa bwana mwenye nyumba angejua ni saa ipi ambayo mwizi angekuja, angekesha na asingeruhusu nyumba yake kuvamiwa.
44Kwa hiyo, pia mnapaswa kuwa tayari, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja katika saa msiyoitarajia.
45Hivyo ni nani aliye mwaminifu, mtumwa mwenye akili, ambaye bwana wake amempa madaraka juu ya walio katika nyumba yake, ili awape chakula kwa wakati unaofaa?
46Amebarikiwa mtumishi huyo, ambaye bwana wake atamkuta akifanya hivyo wakati ajapo.
47Kweli nawaambia kwamba bwana atamweka juu ya kila kitu kilicho chake.
48Lakini kama mtumwa mwovu akisema moyoni mwake, 'Bwana wangu amekawia,'
49na akaanza kuwapiga watumishi wake, na akala na kulewa vileo,
50Bwana wa mtumwa huyo atakuja katika siku ambayo haitarajii, na katika saa ambayo haijui.
51Bwana wake atamkata vipande viwili na kumweka katika nafasi moja sawa na wanafiki, ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.