Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mathayo

Mathayo 22

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Yesu alisema nao tena katika mifano, akisema,
2“Ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme aliyeandaa sherehe ya harusi ya mwanawe.
3Akawatuma watumishi wake kuwakaribisha waliokuwa wamealikwa kuja katika sherehe ya harusi, lakini hawakufika.
4Mfalme aliwatuma tena watumishi wengine, akisema. “Waambieni wote walioalikwa, Angalieni, nimeandaa chakula. Fahali na ndama wangu wanono wamechinjwa, na mambo yote yako tayari, Njoni katika sherehe ya harusi.”
5Lakini watu hao hawakuzingatia kwa dhati mwaliko wake. Baadhi walirejea katika mashamba yao, na wengine walirudi katika sehemu zao za biashara.
6Wengine waliwainukia watumishi wa mfalme na kuwadharirisha na kuwaua.
7Lakini mfalme alikasirika. Alituma jeshi lake, akawaua wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.
8Kisha aliwaambia watumishi wake, “Harusi iko tayari, lakini walioalikwa hawakustahili.
9Kwa hiyo nendeni kwenye makutano ya njia kuu, waalikeni watu wengi kadri iwezekanavyo waje kwenye sherehe ya harusi.”
10Watumishi walienda njia kuu na kuwakaribisha watu wowote waliowaona, wema na wabaya. Hivyo ukumbi wa harusi ulijaa wageni.
11Lakini mfalme alipoingia kuwatazama wageni, alimuona mtu mmoja ambaye hakuvaa vazi rasmi la harusi!
12Mfalme alimwuliza, 'Rafiki, ulipataje kufika hapa ndani bila vazi la harusi?' Na mtu huyo hakujibu chochote.
13Ndipo mfalme alipowaambia watumishi wake, “Mfungeni mtu huyu mikono na miguu na mtupeni nje katika giza, huko ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.
14Kwa kuwa watu wengi wanaitwa, lakini wateule ni wachache.”
15Ndipo Mafarisayo waliondoka na kupanga jinsi ya kumkamata Yesu katika maneno yake mwenyewe.
16Ndipo walipowatuma wanafunzi wao pamoja na Maherode. Na walimwambia Yesu, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mtu wa kweli, na kwamba unafundisha matakwa ya Mungu katika ukweli. Haujali maoni ya mtu mwingine na hauoneshi upendeleo kwa watu.
17Kwa hiyo tuambie, unafikiri nini? Je, ni sahihi kisheria kulipa kodi kwa Kaisari au hapana?”
18Yesu alifahamu uovu wao na akasema, “Kwa nini mnanijaribu, enyi wanafiki?

19Nionesheni pesa itumikayo kulipia kodi.” Ndipo wakamletea dinari.
20Yesu akawauliza, “Sura na jina hili ni vya nani?”
21Wakamjibu, “Vya Kaisari.” Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari vitu vilivyo vyake na vya Mungu mpeni Mungu.”
22Waliposikia hivyo walishangaa. Kisha walimwacha na kwenda zao.
23Siku hiyo baadhi ya Masadukayo walikuja kwa Yesu, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu. Wakamwuliza,
24wakisema, “Mwalimu, Musa alisema, Ikiwa mtu amefariki bila kuzaa watoto, ndugu yake na amrithi huyo mwanamke na ampatie mtoto kwa ajili ya ndugu yake.
25Walikuwapo ndugu saba. Wa kwanza alioa na kisha akafariki bila kuzaa watoto. Akamwachia mke nduguye.
26Kisha ndugu yake wa pili naye akafanya vivyo hivyo, kisha yule wa tatu, ikawa hivyo hadi kwa yule wa saba.
27Baada ya kufanya hivyo wote, yule mwanamke naye alifariki.
28Sasa katika ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani katika ndugu hao saba? Kwa sababu wote walimuoa.”
29Lakina Yesu aliwajibu na kuwaambia, “Mnakosea, kwa sababu hamjui Maandiko wala nguvu za Mungu.
30Kwa kuwa katika ufufuo, watu hawaoi wala kuolewa. Badala yake watu huwa kama malaika huko mbinguni.
31Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjawahi kusoma kile ambacho Mungu alikisema kwenu, akisema,
32Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”
33Wakati kusanyiko waliposikia hili, waliyashangaa mafundisho yake.
34Lakini Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewanyamazisha Masadukayo, walijikusanya wao wenyewe kwa pamoja.
35Mmoja wao, akiwa mwana sheria, alimwuliza swali kwa kumjaribu.
36“Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu kuliko zote katika sheria?”

37Yesu akamjibu, “Lazima umpende Bwana kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.
38Hii ndiyo amri iliyo kuu na ya kwanza.
39Na ya pili inafanana na hiyo- Ni lazima kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.
40Sheria zote na Manabii hutegemea amri hizi mbili.”
41Na Mafarisayo walipokuwa bado wamejikusanya pamoja, Yesu aliwauliza swali.
42Akisema, “J! e, Mwafikiri nini juu ya Kristo? Yeye ni Mwana wa nani?” Nao wakamjibu, “Ni mwana wa Daudi.”
43Yesu akawajibu, “Ni kwa namna gani Daudi katika Roho anamwita Bwana, akisema,
44'Bwana alimwambia Bwana wangu, “Kaa mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowafanya maadui zako wawekwe chini ya miguu yako.”'?”
45Kama Daudi anamwita Kristo “Bwana,” jinsi gani atakuwa mtoto wake?”
46Hakuna aliyeweza kumjibu neno tena, na hakuna aliyethubutu tena kumwuliza maswali zaidi tangu siku hiyo na kuendelea.