19Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe.
20Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia.
21Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, “Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote.
22Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea.
23Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea,
24akaniambia: Paulo usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.
25Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa.
26Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani.”
27Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huku katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu.
28Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arobaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini.
29Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi.
30Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli.
31Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, “Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka.”