Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Yohana 7:13-52 in Swahili (individual language)

Help us?

Yohana 7:13-52 in Biblia Takatifu

13 Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
14 Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza kufundisha.
15 Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema “Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?”
16 Hapo Yesu akawajibu, “Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
17 Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
18 Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.
19 Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
20 Hapo watu wakamjibu, “Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?”
21 Yesu akawajibu, “Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.
22 Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato.
23 Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato?
24 Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki.”
25 Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu?
26 Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?
27 Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!”
28 Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.
29 Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.”
30 Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
31 Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?”
32 Mafarisayo waliwasikia watu wakinong'ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.
33 Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma.
34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika.”
35 Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?
36 Ana maana gani anaposema: Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?”
37 Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, “Aliye na kiu na aje kwangu anywe.
38 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: Anayeniamini mimi, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!”
39 (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.)
40 Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, “Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!”
41 Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine walisema, “Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya?
42 Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!”
43 Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.
44 Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.
45 Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, “Kwa nini hamkumleta?”
46 Walinzi wakawajibu, “Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!”
47 Mafarisayo wakawauliza, “Je, nanyi pia mmedanganyika?
48 Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini?
49 Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!”
50 Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia,
51 “Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?”
52 Nao wakamjibu, “Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!”
Yohana 7 in Biblia Takatifu

Yohana 7:13-52 in Biblia ya Kiswahili

13 Hata hivyo hakuna aliyezungumza wazi juu yake kwa kuwaogopa Wayahudi.
14 Wakati sikukuu ilipofika katikati, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha.
15 Wayahudi walikuwa wakishangaa na kusema, “Kwa jinsi gani mtu huyu anajua mambo mengi? Hajasoma kamwe.”
16 Yesu akawajibu na kuwaambia, “Mafundisho yangu siyo yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
17 Iwapo yeyote atapenda kufanya mapenzi yake yeye, atajua kuhusu mafundisho haya, kama yanatoka kwa Mungu, au kama ninazungumza kutoka kwangu mwenyewe.
18 Kila anayezungumza yatokayo kwake mwenywe hutafuta utukufu wake, bali kila atafutaye utukufu wake yeye aliyemtuma, mtu huyo ni wa kweli, na ndani yake hakuna kutotenda haki.
19 Musa hakuwapa nyinyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja kati yenu atendaye sheria. Kwa nini mnataka kuniua?
20 Makutano wakajibu, “Una pepo. Nani anataka kukuua?”
21 Yesu akajibu na akawaambia, “Nimetenda kazi moja, nanyi nyote mmeshangazwa kwa sababu yake.
22 Musa aliwapa tohara (siyo kwamba inatoka kwa Musa, bali ile inatoka kwa mababa), na katika Sabato mnamtahili mtu.
23 Iwapo mtu atapokea tohara katika siku ya Sabato ili kwamba sheria ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia mimi kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa katika Sabato?
24 Msihukumu kulingana na mwonekano, bali hukumuni kwa haki.
25 Baadhi yao kutoka Yerusalemu wakasema, “Siye huyu wanayemtafuta kumwua?
26 Na tazama, anaongea wazi wazi, na hawasemi chochote juu yake. Haiwezi ikawa kwamba viongozi wanajua kweli kuwa huyu ni Kristo, inaweza kuwa?
27 Tunajua huyu mtu anatokea wapi. Kristo atakapokuja, hata hivyo, hakuna atakayejua wapi anakotoka.”
28 Yesu alikuwa akipaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, “Ninyi nyote mnanijua mimi na mnajua nitokako. Sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye aliyenituma ni wa kweli, na hamumjui yeye.
29 Ninamjua yeye kwa sababu nimetoka kwake na alinituma.”
30 Walikuwa wanajaribu kumkamata, lakini hakuna hata mmoja aliyeinua mkono wake juu yake kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijafika.
31 Hata hivyo, wengi katika makutano walimwamini. Walisema, “Kristo atakapokuja, atafanya ishara nyingi kuliko alizofanya mtu huyu?”
32 Mafarisayo waliwasikia makutano wakinong'onezana mambo haya kuhusu Yesu, na wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma maafisa ili kumkamata.
33 Ndipo Yesu aliposema, “Bado kuna muda kitambo niko pamoja nanyi, na baadaye nitakwenda kwake yeye aliyenituma.
34 Mtanitafuta wala hamtaniona; kule niendako, hamtaweza kuja.”
35 Kwa hiyo Wayahudi wakasemezana wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi kwamba tusiweze kumuona? Ataenda kwa Waliotawanyika kati ya Wayunani na kuwafundisha Wayunani?
36 Ni neno gani hili alilolisema, 'Mtanitafuta wala hamtaniona; kule niendako hamtamweza kuja'?”
37 Sasa katika siku ya mwisho, siku kubwa ya sikukuu, Yesu alisimama akapaza sauti, akisema, “Ikiwa yeyote ana kiu, na aje kwangu anywe.
38 Yeye aniaminiye mimi, kama maandiko yalivyosema, kutoka ndani yake itatiririka mito ya maji ya uzima.”
39 Lakini aliyasema haya kuhusu Roho, ambaye wao wamwaminio watampokea; Roho alikuwa bado hajatolewa kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.
40 Baadhi ya makutano, waliposikia maneno haya, walisema, “Kweli huyu ni nabii.”
41 Wengine walisema, “Huyu ni Kristo.” Lakini wengine walisema, “nini, Kristo aweza kutoka Galilaya?
42 Maandiko hayajasema kuwa Kristo atatokea katika ukoo wa Daudi na kutoka Bethlehemu, kijiji ambacho Daudi alikuwa?
43 Hivyo, pale ukainuka mgawanyiko katikati ya makutano kwa ajili yake.
44 Wengine kati yao wangelimkamata, lakini hakuna aliyenyoosha mikono yake juu yake.
45 Ndipo wale maofisa wakarudi kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, nao wakawaambia, “Kwa nini hamjamleta?”
46 Maofisa wakajibu, “Hakuna mtu aliyewahi kuzungumza kama huyu kabla.”
47 Ndipo Mafarisayo walipowajibu, “Na nyinyi pia mmepotoshwa?
48 Kuna yeyote kati ya watawala anayemwamini, au yeyote wa Mafarisayo?
49 Bali hawa makutano wasiojua sheria - wamelaaniwa.”
50 Nikodemo akawaambia (yeye aliyemwendea Yesu zamani, akiwa mmoja wa Mafarisayo),
51 “Je sheria yetu inamhukumu mtu isipokuwa amesikilizwa kwanza na kujua anachokifanya?”
52 Walijibu na kumwambia, “Na wewe pia unatokea Galilaya? Tafuta na uone kwamba hakuna nabii aliyetokea Galilaya.”
Yohana 7 in Biblia ya Kiswahili