30 Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
31 Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, ule chakula.”
32 Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.”
33 Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?”
34 Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
35 Ninyi mwasema: Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika! Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.
36 Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
37 Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: Mmoja hupanda na mwingine huvuna.