7 Usishangae kwa sababu nilikuwambia, 'ni lazima kuzaliwa mara ya pili.'
8 Upepo huvuma popote upendapo na sauti yake mwaisikia, lakini hamjui utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo hali ya kila aliyezaliwa na roho.
9 Nikodemo akajibu, kwa kusema, “Mambo haya yawezekanaje?”
10 Yesu akamjibu, “Wewe u mwalimu wa Israeli, hata hauyajui mambo haya?
11 Amini, amini, nakuambia, kile tunachokifahamu twakishuhudia kwa kile tulichokiona. Lakini hampokei ushuhuda wetu.
12 Kama nimewambia mambo ya hapa duniani na hamuamini, mtawezaje kuamini kama nikiwambia mambo ya mbinguni?
13 Maana hakuna aliyepanda juu kutoka mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka, Mwana wa Adamu.
14 Kama vile Musa alivyomwinua nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu lazima ainuliwe,
15 ili kwamba wote watakaomwamini wapate uzima wa milele.
16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, kwamba akamtoa mwanae wa pekee, ili kwamba mtu yeyote amwaminiye asiangamie bali awe na uzima wa milele.
17 Kwa sababu Mungu hakumtuma mwanae duniani ili auhukumu ulimwengu, bali kwamba ulimwengu uokolewe katika yeye.
18 Amwaminiye Yeye hatahukumiwa. Yeye asiyemwamini tayari ameshahukumiwa kwa sababu hajaliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
19 Hii ndiyo sababu ya hukumu, ya kwamba nuru imekuja ulimwenguni, lakini wanadamu wakapenda giza zaidi ya nuru kwa sababu matendo yao yalikuwa maovu.
20 kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru wala haji nuruni ili matendo yake yasije yakawekwa wazi.
21 Lakini, yeye atendaye kweli huja kwenye nuru ili matendo yake yaonekane kwamba yametendwa kwa utiifu wa Mungu.