23 Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono.
24 Basi, hao askari wakashauriana: “Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani.” Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: “Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura.” Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.
25 Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene.
26 Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.”
27 Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
28 Yesu alijua kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.”
29 Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni.
30 Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainama kichwa, akatoa roho.
31 Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe.
32 Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu.
33 Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja miguu.