Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Yohana 12:2-39 in Swahili (individual language)

Help us?

Yohana 12:2-39 in Biblia Takatifu

2 Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu.
3 Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi.
4 Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
5 “Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa maskini?”
6 Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.
7 Lakini Yesu akasema, “Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.
8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote.”
9 Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.
10 Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro,
11 Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
12 Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.
13 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: “Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli.”
14 Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
15 “Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda.”
16 Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
17 Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia.
18 Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.
19 Basi, Mafarisayo wakaambiana, “Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata.”
20 Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.
21 Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.”
22 Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.
23 Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!
24 Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.
25 Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele.
26 Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
27 “Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: Baba, usiruhusu saa hii inifikie? Lakini ndiyo maana nimekuja—ili nipite katika saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.”
29 Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Malaika ameongea naye!”
30 Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.
31 Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.
32 Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.”
33 (Kwa kusema hivyo alionyesha atakufa kifo gani).
34 Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?”
35 Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.
36 Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
37 Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini.
38 Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: “Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?”
39 Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema:
Yohana 12 in Biblia Takatifu

Yohana 12:2-39 in Biblia ya Kiswahili

2 Basi wakamwandalia chakula cha jioni huko, na Martha akamtumikia, wakati huo Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu.
3 Kisha Mariamu akachukua ratli ya manukato yaliyotengenezwa kwa nardo safi, yenye thamani kubwa, akampaka Yesu miguuni, na kumfuta miguu kwa nywele zake; nyumba yote ilijaa harufu ya manukato.
4 Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi wake, ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
5 “Kwanini manukato haya yasingeuzwa kwa dinari mia tatu na wakapewa maskini?”
6 Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini, bali kwa sababu alikuwa mwizi: yeye ndiye aliyeshika mfuko wa fedha na alikuwa anachukua baadhi ya vilivyowekwa humo kwa ajili yake mwenyewe.
7 Yesu alisema, “Mwache aweke alicho nacho kwa ajili ya siku ya maziko yangu.
8 Maskini mtakuwa nao siku zote; lakini hamtakuwa nami siku zote.”
9 Basi umati mkubwa wa Wayahudi walipata kujua ya kuwa Yesu yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili ya Yesu tu, ila wamwone na Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka katika wafu.
10 Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri ili wamue Lazaro;
11 maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walienda zao na wakamwamini Yesu.
12 Na siku ya pili yake umati mkubwa walikuja kwenye sikukuu. Waliposikia ya kuwa Yesu anakuja Yerusalemu,
13 walichukua matawi ya miti ya mitende na kutoka nje kwenda kumlaki na wakapiga kelele, “Hosana! Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli.”
14 Yesu alimpata mwana-punda akampanda; kama vile ilivyoandikwa,
15 “Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.”
16 Wanafunzi wake hawakuyaelewa mambo haya hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kuwa mambo haya aliandikiwa yeye na ya kwamba wametenda mambo haya kwake.
17 Basi lile kundi la watu waliokuwepo pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, wakashuhudia kwa wengine.
18 Na ilikuwa kwa sababu hii pia kwamba kundi la watu walikwenda kumlaki kwasababu walisikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo.
19 Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, “Tazama, sasa hamwezi kufanya lolote; tazama, ulimwengu umekwenda kwake.”
20 Sasa baadhi ya Wayunani walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakienda kuabudu kwenye sikukuu.
21 Hawa walimwendea Filipo, ambaye alitoka Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba wakisema, “Bwana, sisi tunatamani kumwona Yesu.”
22 Filipo akaenda akamwambia Andrea; Andrea na Filipo wakaenda na kumwambia Yesu.
23 Yesu akawajibu akasema, “Saa imefika kwa ajili ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
24 Amini, amini, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, itazaa matunda mengi.
25 Yeye apendaye uhai wake ataupoteza; bali yeye auchukiaye uhai wake katika ulimemngu huu atausalimisha hata uzima wa milele.
26 Mtu yeyote akinitumikia mimi, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Mtu yeyote akinitumikia, Baba atamheshimu.
27 Sasa roho yangu imefadhaika: nami nisemeje? 'Baba, uniokoe katika saa hii'? Lakini ni kwa kusudi hii nimeifikia saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako.” Kisha sauti ikaja kutoka mbinguni na kusema, “Nimelitukuza nami nitalitukuza tena.”
29 Basi mkutano uliosimama karibu naye wakasikia, wakasema ya kwamba kumekuwa ngurumo. Wengine walisema, “Malaika amesema naye.”
30 Yesu akajibu na kusema, “Sauti hii haikuja kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
31 Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo: Sasa mkuu wa ulimwngu huu atatupwa nje.
32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.”
33 Aliyanena hayo akionesha ni mauti gani atakayokufa.
34 Mkutano wakamjibu, “Sisi tumesikia katika sheria ya kwamba Kristo atadumu hata milele. Nawe wasemaje, 'Mwana Adamu lazima ainuliwe juu'? Huyu Mwana wa Mtu ni nani?”
35 Basi Yesu akawaambia, “Nuru ingalipo pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru, ili kwamba giza lisije likawaweza. Yeye aendaye gizani hajui aendako.
36 Mngali mnayo nuru, iaminini nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Yesu aliyasema haya na kisha akaenda zake akajificha wasimwone.
37 Ingawa Yesu alifanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, bado hawakumwamini
38 ili litimie neno la nabii Isaya, alilosema: “Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?”
39 Ndio sababu wao hawakuamini, maana Isaya alisema tena,
Yohana 12 in Biblia ya Kiswahili