Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Warumi 8:2-30 in Swahili (individual language)

Help us?

Warumi 8:2-30 in Biblia Takatifu

2 Maana, sheria ya Roho iletayo uzima kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo.
3 Mungu ametekeleza jambo lile ambalo Sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu w binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi.
4 Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya Sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho.
5 Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho.
6 Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uzima na amani.
7 Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii.
8 Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Lakini ninyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo.
10 Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu itakufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmekubaliwa kuwa waadilifu.
11 Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka wafu ataipa uzima miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
12 Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu.
13 Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi.
14 Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu.
15 Kwa maana, Roho mliyempokea si Roho mwenye kuwafanya ninyi watumwa na kuwatia tena hofu; sivyo, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya ninyi watoto wa Mungu, na kwa nguvu ya huyo Roho, sisi tunaweza kumwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!”
16 Naye Roho mwenyewe anajiunga na roho zetu na kuthibitisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu.
17 Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.
18 Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyafananisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu.
19 Viumbe vyote vinatazamia kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake.
20 Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini,
21 maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto.
23 Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukitazamia kufanywa watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe.
24 Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa; lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona?
25 Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu.
26 Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka.
27 Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.
28 Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake.
29 Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
30 Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita aliwakubali kuwa waadilifu; na hao aliowakubali kuwa waadilifu aliwashirikisha pia utukufu wake.
Warumi 8 in Biblia Takatifu

Warumi 8:2-30 in Biblia ya Kiswahili

2 Kwa kuwa kanuni ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imenifanya mimi kuwa huru mbali na kanuni ya dhambi na mauti.
3 Kwa maana kile ambacho sheria ilishindwa kufanya kwa sababu ilikuwa dhaifu katika mwili, Mungu alifanya. Alimtuma Mwana wake wa pekee kwa mfano wa mwili wa dhambi awe sadaka ya dhambi, na akaihukumu dhambi katika mwili.
4 Alifanya hivi ili maagizo ya sheria yatimilizwe ndani yetu, sisi tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali kwa kufuata mambo ya Roho.
5 Wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili, lakini wale waifuatao Roho huyafikiri mambo ya Roho.
6 Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti, bali nia ya Roho ni uzima na amani.
7 Hii ni kwa sababu ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.
8 Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Hata hivyo, hampo katika mwili bali katika Roho, kama ni kweli kwamba Roho wa Mungu huishi ndani yenu. Lakini kama mtu hana Roho wa Kristo, yeye si wake.
10 Kama Kristo yumo ndani yenu, mwili umekufa kwa mambo ya dhambi, bali roho ni hai kwa mambo ya haki.
11 Ikiwa Roho wa yule aliyemfufua Yesu kutoka wafu huishi ndani yenu, yeye yule aliyemfufua Kristo kutoka katika wafu ataipa pia miili yenu ya mauti uhai kwa njia ya Roho wake, aishie ndani yenu.
12 Hivyo basi, ndugu zangu, sisi tu wadeni, lakini si kwa mwili kwamba tuishi kwa jinsi ya mwili.
13 Maana ikiwa mnaishi kwa jinsi ya mwili, mpo karibu kufa, lakini ikiwa kwa Roho mnayafisha matendo ya mwili, nanyi mtaishi.
14 Maana kama ambavyo wengi wanaongozwa na Roho wa Mungu, hawa ni wana wa Mungu.
15 Kwa kuwa hamkupokea roho wa utumwa tena hata muogope. Badala yake, mlipokea roho ya kufanywa kuwa wana, ambayo kwayo tunalia, “Abba, Baba!”
16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa tu watoto wa Mungu.
17 Ikiwa tu watoto, basi tu warithi pia, warithi wa Mungu. Na sisi tu warithi pamoja na Kristo, ikiwa kwa kweli tunateseka na yeye ili tupate kutukuzwa pamoja naye.
18 Kwa kuwa nayahesabu mateso ya wakati huu kuwa si kitu nikilinganisha na utukufu utakaofunuliwa kwetu.
19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
20 Kwa maana uumbaji pia ulitiishwa chini ya ubatili, si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha. Ni katika tumaini
21 kwamba uumbaji wenyewe nao utawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, na kuingizwa katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa uumbaji nao pia unaugua na kuteseka kwa uchungu pamoja hata sasa.
23 Si hivyo tu, ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho - sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukisubiri kufanywa wana, yaani ukombozi wa miili yetu.
24 Kwa maana ni kwa taraja hili tuliokolewa. Lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana hakuna taraja tena, kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho?
25 Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.
26 Kwa jinsi iyo hiyo, Roho naye hutusaidia katika udhaifu wetu. Kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
27 Na yeye aichunguzaye mioyo huijua akili ya Roho, kwa sababu huomba kwa niaba yao walioamini kulingana na mapenzi ya Mungu.
28 Nasi twajua ya kuwa kwa wote wampendao Mungu, yeye hufanya mambo yote pamoja kwa wema, kwa wale wote walioitwa kwa kusudi lake.
29 Kwa sababu wale wote aliowajua tangu asili, pia aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miogoni mwa ndugu wengi.
30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao aliwaita pia. Na wale aliowaita, hao aliwahesabia haki. Na wale aliowahesabia haki, hao pia akawatukuza.
Warumi 8 in Biblia ya Kiswahili