Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Warumi - Warumi 8

Warumi 8:2-30

Help us?
Click on verse(s) to share them!
2Kwa kuwa kanuni ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imenifanya mimi kuwa huru mbali na kanuni ya dhambi na mauti.
3Kwa maana kile ambacho sheria ilishindwa kufanya kwa sababu ilikuwa dhaifu katika mwili, Mungu alifanya. Alimtuma Mwana wake wa pekee kwa mfano wa mwili wa dhambi awe sadaka ya dhambi, na akaihukumu dhambi katika mwili.
4Alifanya hivi ili maagizo ya sheria yatimilizwe ndani yetu, sisi tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali kwa kufuata mambo ya Roho.
5Wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili, lakini wale waifuatao Roho huyafikiri mambo ya Roho.
6Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti, bali nia ya Roho ni uzima na amani.
7Hii ni kwa sababu ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.
8Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
9Hata hivyo, hampo katika mwili bali katika Roho, kama ni kweli kwamba Roho wa Mungu huishi ndani yenu. Lakini kama mtu hana Roho wa Kristo, yeye si wake.
10Kama Kristo yumo ndani yenu, mwili umekufa kwa mambo ya dhambi, bali roho ni hai kwa mambo ya haki.
11Ikiwa Roho wa yule aliyemfufua Yesu kutoka wafu huishi ndani yenu, yeye yule aliyemfufua Kristo kutoka katika wafu ataipa pia miili yenu ya mauti uhai kwa njia ya Roho wake, aishie ndani yenu.
12Hivyo basi, ndugu zangu, sisi tu wadeni, lakini si kwa mwili kwamba tuishi kwa jinsi ya mwili.
13Maana ikiwa mnaishi kwa jinsi ya mwili, mpo karibu kufa, lakini ikiwa kwa Roho mnayafisha matendo ya mwili, nanyi mtaishi.
14Maana kama ambavyo wengi wanaongozwa na Roho wa Mungu, hawa ni wana wa Mungu.
15Kwa kuwa hamkupokea roho wa utumwa tena hata muogope. Badala yake, mlipokea roho ya kufanywa kuwa wana, ambayo kwayo tunalia, “Abba, Baba!”
16Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa tu watoto wa Mungu.
17Ikiwa tu watoto, basi tu warithi pia, warithi wa Mungu. Na sisi tu warithi pamoja na Kristo, ikiwa kwa kweli tunateseka na yeye ili tupate kutukuzwa pamoja naye.
18Kwa kuwa nayahesabu mateso ya wakati huu kuwa si kitu nikilinganisha na utukufu utakaofunuliwa kwetu.
19Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
20Kwa maana uumbaji pia ulitiishwa chini ya ubatili, si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha. Ni katika tumaini
21kwamba uumbaji wenyewe nao utawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, na kuingizwa katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22Kwa maana twajua ya kuwa uumbaji nao pia unaugua na kuteseka kwa uchungu pamoja hata sasa.
23Si hivyo tu, ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho - sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukisubiri kufanywa wana, yaani ukombozi wa miili yetu.
24Kwa maana ni kwa taraja hili tuliokolewa. Lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana hakuna taraja tena, kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho?
25Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.
26Kwa jinsi iyo hiyo, Roho naye hutusaidia katika udhaifu wetu. Kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
27Na yeye aichunguzaye mioyo huijua akili ya Roho, kwa sababu huomba kwa niaba yao walioamini kulingana na mapenzi ya Mungu.
28Nasi twajua ya kuwa kwa wote wampendao Mungu, yeye hufanya mambo yote pamoja kwa wema, kwa wale wote walioitwa kwa kusudi lake.
29Kwa sababu wale wote aliowajua tangu asili, pia aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miogoni mwa ndugu wengi.
30Na wale aliowachagua tangu asili, hao aliwaita pia. Na wale aliowaita, hao aliwahesabia haki. Na wale aliowahesabia haki, hao pia akawatukuza.

Read Warumi 8Warumi 8
Compare Warumi 8:2-30Warumi 8:2-30