Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Warumi 4:1-24 in Swahili (individual language)

Help us?

Warumi 4:1-24 in Biblia Takatifu

1 Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu?
2 Kama Abrahamu alikubaliwa kuwa mwadilifu kutokana na matendo yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu.
3 Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.”
4 Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake.
5 Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, na hivi humkubali kuwa mwadilifu.
6 Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake:
7 “Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa.
8 Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.”
9 Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.”
10 Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa.
11 Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu.
12 Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.
13 Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii Sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu.
14 Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii Sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu.
15 Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna Sheria, haiwezekani kuivunja.
16 Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: si kwa wale tu wanaoishika Sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote.
17 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini—Mungu ambaye huwapa wafu uzima, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa.
18 Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Wazao wako watakuwa wengi kama nyota!”
19 Alikuwa mzee wa karibu miaka mia moja, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa.
20 Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu.
21 Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi.
22 Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu.
23 Inaposemwa, “Alimkubali,” haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu.
24 Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka wafu.
Warumi 4 in Biblia Takatifu

Warumi 4:1-24 in Biblia ya Kiswahili

1 Tutasema nini tena kwamba Abrahamu, baba yetu kwa jinsi ya mwili, amepatikana?
2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, angekuwa na sababu ya kujisifu, lakini si mbele za Mungu.
3 Kwani maandiko yanasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
4 Sasa kwa mtu afanyaye kazi, malipo yake hayahesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtaua, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
6 Daudi pia hunena baraka juu ya mtu ambaye Mungu amhesabia haki pasipo matendo.
7 Alisema, “Wamebarikiwa wale ambao maovu yao yamesamehewa na ambao dhambi zao zimefunikwa.
8 Amebarikiwa mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.”
9 Basi je baraka hizi ni kwa wale waliotahiriwa tu, au pia kwa wale wasiotahiriwa? Kwa maana twasema, “kwa Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.”
10 Hivyo ilihesabiwaje basi? Wakati Abrahamu alikuwa katika tohara, au kabla hajatahiriwa? Haikuwa katika kutahiriwa, bali katika kutotahiriwa.
11 Abrahamu alipokea alama ya kutahiriwa. Huu ulikuwa muhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo tayari kabla hajatahiriwa. Matokeo ya ishara hii ni kwamba alifanyika kuwa baba wa wote waaminio, hata kama wapo katika kutotahiriwa. Hii ina maana kwamba haki itahesabiwa kwao.
12 Hii pia ilimaanisha kuwa Abrahamu alifanyika baba wa tohara si tu kwa wale wanaotokana na tohara, bali pia wale wanaozifuata nyayo za baba yetu Abrahamu. Na hii ndiyo imani aliyokuwa nayo kwa wasiotahiriwa.
13 Kwa maana haikuwa kwa sheria kwamba ahadi ilitolewa kwa Abrahamu na uzao wake, ahadi hii ya kwamba watakuwa warithi wa dunia. isipokuwa, ilikuwa kupitia haki ya imani.
14 Kwa maana kama wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.
15 Kwa sababu sheria huleta ghadhabu, lakini pale ambapo hakuna sheria, pia hakuna kutotii.
16 Kwa sababu hii hili hutokea kwa imani, ili iwe kwa neema. Matokeo yake, ahadi ni dhahiri kwa uzao wote. Na wazawa hawa si tu wale wanaojua sheria, bali pia wale ambao ni wa imani ya Abrahamu. Kwa maana yeye ni baba yetu sisi sote,
17 kama ilivyoandikwa, “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Abrahamu alikuwa katika uwepo wa yule aliyemwamini, yaani, Mungu ambaye huwapa wafu uzima na kuyaita mambo ambayo hayapo ili yaweze kuwepo.
18 Licha ya hali zote za nje, Abrahamu kwa ujasiri alimuamini Mungu kwa siku zijazo. Hivyo akawa baba wa mataifa mengi, kulingana na kile kilichonenwa,”... Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”
19 Yeye hakuwa dhaifu katika imani. Abrahamu alikiri kwamba mwili wake mwenyewe ulikwisha kufa - alikuwa na umri wa karibu miaka mia moja. Pia alikubaliana na hali ya kufa ya tumbo la Sara.
20 Lakini kwa sababu ya ahadi ya Mungu, Abrahamu hakusita katika kutokuamini. Bali, alitiwa nguvu katika imani na alimsifu Mungu.
21 Alikuwa akijua hakika ya kuwa kile ambacho Mungu ameahidi, alikuwa pia na uwezo wa kukikamilisha.
22 Kwa hiyo hii pia ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
23 Sasa haikuandikwa tu kwa faida yake, kwamba ilihesabiwa kwake.
24 Iliandikwa kwa ajili yetu pia, kwa waliowekewa kuhesabiwa, sisi ambao tunaamini katika yeye aliyemfufua Bwana wetu Yesu kutoka wafu.
Warumi 4 in Biblia ya Kiswahili