Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Warumi - Warumi 4

Warumi 4:1-24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Tutasema nini tena kwamba Abrahamu, baba yetu kwa jinsi ya mwili, amepatikana?
2Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, angekuwa na sababu ya kujisifu, lakini si mbele za Mungu.
3Kwani maandiko yanasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
4Sasa kwa mtu afanyaye kazi, malipo yake hayahesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
5Lakini kwa mtu asiyefanya kazi bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtaua, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
6Daudi pia hunena baraka juu ya mtu ambaye Mungu amhesabia haki pasipo matendo.
7Alisema, “Wamebarikiwa wale ambao maovu yao yamesamehewa na ambao dhambi zao zimefunikwa.
8Amebarikiwa mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.”
9Basi je baraka hizi ni kwa wale waliotahiriwa tu, au pia kwa wale wasiotahiriwa? Kwa maana twasema, “kwa Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.”
10Hivyo ilihesabiwaje basi? Wakati Abrahamu alikuwa katika tohara, au kabla hajatahiriwa? Haikuwa katika kutahiriwa, bali katika kutotahiriwa.
11Abrahamu alipokea alama ya kutahiriwa. Huu ulikuwa muhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo tayari kabla hajatahiriwa. Matokeo ya ishara hii ni kwamba alifanyika kuwa baba wa wote waaminio, hata kama wapo katika kutotahiriwa. Hii ina maana kwamba haki itahesabiwa kwao.
12Hii pia ilimaanisha kuwa Abrahamu alifanyika baba wa tohara si tu kwa wale wanaotokana na tohara, bali pia wale wanaozifuata nyayo za baba yetu Abrahamu. Na hii ndiyo imani aliyokuwa nayo kwa wasiotahiriwa.
13Kwa maana haikuwa kwa sheria kwamba ahadi ilitolewa kwa Abrahamu na uzao wake, ahadi hii ya kwamba watakuwa warithi wa dunia. isipokuwa, ilikuwa kupitia haki ya imani.
14Kwa maana kama wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.
15Kwa sababu sheria huleta ghadhabu, lakini pale ambapo hakuna sheria, pia hakuna kutotii.
16Kwa sababu hii hili hutokea kwa imani, ili iwe kwa neema. Matokeo yake, ahadi ni dhahiri kwa uzao wote. Na wazawa hawa si tu wale wanaojua sheria, bali pia wale ambao ni wa imani ya Abrahamu. Kwa maana yeye ni baba yetu sisi sote,
17kama ilivyoandikwa, “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Abrahamu alikuwa katika uwepo wa yule aliyemwamini, yaani, Mungu ambaye huwapa wafu uzima na kuyaita mambo ambayo hayapo ili yaweze kuwepo.
18Licha ya hali zote za nje, Abrahamu kwa ujasiri alimuamini Mungu kwa siku zijazo. Hivyo akawa baba wa mataifa mengi, kulingana na kile kilichonenwa,”... Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”
19Yeye hakuwa dhaifu katika imani. Abrahamu alikiri kwamba mwili wake mwenyewe ulikwisha kufa - alikuwa na umri wa karibu miaka mia moja. Pia alikubaliana na hali ya kufa ya tumbo la Sara.
20Lakini kwa sababu ya ahadi ya Mungu, Abrahamu hakusita katika kutokuamini. Bali, alitiwa nguvu katika imani na alimsifu Mungu.
21Alikuwa akijua hakika ya kuwa kile ambacho Mungu ameahidi, alikuwa pia na uwezo wa kukikamilisha.
22Kwa hiyo hii pia ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
23Sasa haikuandikwa tu kwa faida yake, kwamba ilihesabiwa kwake.
24Iliandikwa kwa ajili yetu pia, kwa waliowekewa kuhesabiwa, sisi ambao tunaamini katika yeye aliyemfufua Bwana wetu Yesu kutoka wafu.

Read Warumi 4Warumi 4
Compare Warumi 4:1-24Warumi 4:1-24