1Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa kuwa mbingu ya kwanza na nchi ya kwanza zimekwishapita, na bahari haikuwepo tena.
2Niliona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ambao ulikuja chini kutoka mbinguni kwa Mungu, ulioandaliwa kama bibi harusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.
3Nilisikia sauti kubwa kutoka kwenye kiti cha enzi ikisema, “Tazama! Makao ya Mungu yapo pamoja na wanadamu, naye ataishi pamoja nao. Watakuwa watu wake, na Mungu mwenyewe atakuwa nao na atakuwa Mungu wao.
4Atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na hapatakuwa na kifo tena, au kuomboleza, au kulia, au maumivu. Mambo ya zamani yamekwishakupita.
5Yeye ambaye alikuwa ameketi juu ya kiti cha enzi alisema, “Tazama! Nafanya mambo yote kuwa mapya.” Alisema, “Andika hili kwa sababu maneno haya ni ya hakika na kweli.”
6Aliniambia, “Mambo haya yalikwisha kupita! Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho. Kwa yeyote aonaye kiu nitampatia kinywaji bila gharama kutoka katika chemchemi za maji ya uzima.
7Yeye ashindaye atayarithi mambo haya, na nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
8Lakini kama ilivyo kwa waoga, wasioamini, wachukizao, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, sehemu yao itakuwa katika ziwa la moto wa kiberiti uunguzao. Hiyo ndiyo mauti ya pili.”
9Mmoja wa malaika saba alikuja kwangu, mmoja ambaye alikuwa na mabakuli saba yaliyojaa mapigo saba ya mwisho na alisema, “Njoo hapa. Nitakuonesha bibi harusi, mke wa mwana kondoo.”
10Kisha alinichukua mbali katika Roho kwenye mlima mkubwa na mrefu na alinionesha mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka chini kutoka mbinguni kwa Mungu.
11Yerusalemu ulikuwa na utukufu wa Mungu, na uzuri wake ulikuwa kama kito cha thamani, kama jiwe la kioo safi la yaspi.
12Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye milango kumi na miwili, pamoja na malaika kumi na wawili milangoni. Juu ya milango palikuwa pameandikwa majina ya makabila kumi na mawili ya wana wa Israeli.
13Upande wa mashariki palikuwa na milango mitatu, upande wa kusini milango mitatu, upande wa kaskazini milango mitatu, na upande wa magharibi milango mitatu.
14Kuta za mji zilikuwa na misingi kumi na miwili, na juu yake palikuwa na majina kumi na mawili ya mitume kumi na wawili wa Mwana Kondoo.
15Mmoja aliyeongea nami alikuwa na kipimo cha fimbo iliyotengenezwa kwa dhahabu kwa ajili ya kupima mji, milango yake na kuta zake.
16Mji uliwekwa ndani ya mraba; urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Alipima mji kwa kipimio cha fimbo, stadia 12, 000 kwa urefu (urefu wake, upana, na kimo vilifanana).
17Vilevile alipima ukuta wake, unene wake ulikuwa dhiraa 144 kwa vipimo vya kibinadamu (ambavyo pia ni vipimo vya malaika).
18Ukuta ulikuwa umejengwa kwa yaspi na mji wenye dhahabu safi, kama kioo safi.
19Misingi ya ukuta ilikuwa imepambwa na kila aina ya jiwe la thamani. La kwanza lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedon, la nne zumaridi,
20la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolitho, la nane zabarajadi, la tisa yakuti ya manjano, la kumi krisopraso, la kumi na moja hiakintho, la kumi na mbili amethisto.
21Milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili, kila mlango ulitengenezwa kutoka kwenye lulu moja. Mitaa ya mji ilikuwa dhahabu safi, ikionekana kama kioo safi.
22Sikuona hekalu lolote ndani ya mji, kwa kuwa Bwana Mungu, ambaye anatawala juu ya vyote, na Mwana Kondoo ni hekalu lake.
23Mji haukuhitaji jua au mwezi ili kungaza juu yake kwa sababu utukufu wa Mungu uliangaza juu yake, na taa yake ni Mwana Kondoo.
24Mataifa watatembea kwa mwanga wa mji huo. Wafalme wa dunia wataleta fahari zao ndani yake.
25Milango yake haitafungwa wakati wa mchana, na hapatakuwa na usiku pale.
26Wataleta fahari na heshima ya mataifa ndani yake,
27na hakuna kichafu kitakachoingia ndani yake. Wala yeyote ambaye afanyaye jambo lolote la aibu au udanganyifu hataingia, bali ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana Kondoo.