1Baada ya mambo haya nilisikia sauti kama ya mlio mkubwa wa kundi kubwa la watu mbinguni ikisema, “Haleluya. Wokovu, utukufu, na nguvu ni vya Mungu wetu.
2Hukumu zake ni kweli na za haki, kwa kuwa amemhukumu kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uzinzi wake. Amefanya kisasi kwa damu ya watumishi wake, ambayo aliimwaga yeye mwenyewe.”
3Kwa mara ya pili walisema, “Haleluya! Moshi hutoka kwake milele na milele.”
4Wale wazee ishirini na wanne na viumbe hai wanne wakasujudu na kumwabudu Mungu akaaye kwenye kiti cha enzi. Walikuwa wakisema, “Amina. Haleluya!”
5Ndipo sauti ilitoka kwenye kiti cha enzi, ikisema, “Msifuni Mungu wetu, enyi watumishi wake wote, ninyi mnaomcha yeye, wote wasio na umuhimu na wenye nguvu.”
6Ndipo nilisikia sauti kama sauti ya kundi kubwa la watu, kama sauti ya ngurumo ya maji mengi, na kama ngurumo ya radi, ikisema, “Haleluya! Bwana ni Mungu wetu, mtawala juu ya wote, hutawala.
7Na tushangilie na kufurahi na kumpa utukufu kwa sababu harusi na sherehe ya Mwana Kondoo imekuja, na bibi harusi yuko tayari.”
8Aliruhusiwa kuvalishwa kitani safi na yenye kung'aa (kitani safi ni matendo ya haki ya waumini).
9Malaika akasema nami, “Yaandike haya: Wamebarikiwa walioalikwa kwenye sherehe ya harusi ya Mwana kondoo.” Vilevile akaniambia, “Haya ni maneno ya kweli ya Mungu.”
10Nilisujudu mbele ya miguu yake nikamwabudu, lakini akaniambia, “Usifanye hivi! Mimi ni mtumishi mwenzako na wa ndugu zako mwenye kuushika ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu, kwa kuwa ushuhuda wa Yesu ni roho ya unabii.”
11Kisha niliona mbingu zimefunguka, na tazama kulikuwa na farasi mweupe! Na yule aliyekuwa amempanda anaitwa Mwaminifu na wa Kweli. Huhukumu kwa haki na kufanya vita.
12Macho yake ni kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake ana taji nyingi. Ana jina lililoandikwa juu yake asilolifahamu mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe.
13Amevaa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aliitwa Neno la Mungu.
14Majeshi ya mbinguni yalikuwa yakimfuata juu ya farasi weupe, walivalishwa kitani nzuri, nyeupe na safi.
15Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao huyaangamiza mataifa, naye atawatawala kwa fimbo ya chuma. Naye hukanyaga vyombo vya mvinyo kwa hasira kali ya Mungu, hutawala juu ya wote.
16Naye ameandikwa juu ya vazi lake na katika paja lake jina, MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA.
17Niliona malaika amesimama katika jua. Aliwaita kwa sauti kuu ndege wote warukao juu, “Njoni, kusanyikeni pamoja kwenye chakula kikuu cha Mungu.
18Njoni mle nyama ya wafalme, nyama ya majemedari, nyama ya watu wakubwa, nyama ya farasi na wapanda farasi, na nyama ya watu wote, walio huru na watumwa, wasio na umuhimu na wenye nguvu.”
19Nilimwona mnyama na wafalme wa nchi pamoja na majeshi yao. Walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kufanya vita na mmoja aliyepanda farasi na jeshi lake.
20Mnyama alikamatwa na nabii wake wa uongo aliyezifanya ishara katika uwepo wake. Kwa ishara hizi aliwadanganya wale walioipokea chapa ya mnyama na walioisujudia sanamu yake. Wote wawili walitupwa wangali hai katika ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.
21Wale waliobaki waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa mmoja aliyepanda juu ya farasi. Ndege wote walikula mizoga ya miili yao.