1Jina zuri ni bora kuliko manukato ya gharama, na siku ya kufa ni bora kuliko siku ya kuzaliwa.
2Ni bora kwenda kwenye nyumba ya maombolezo kuliko nyumba ya karamu, kwa kuwa maombolezo huja kwa watu wote wakati wa mwisho wa uhai, kwa hiyo watu wanaoishi ni lazima waweke hili moyoni.
3Huzuni ni bora kuliko kicheko, kwa kuwa baada ya uso wa huzuni huja furaha ya moyo.
4Moyo wa mwenye hekima uko katika nyumba ya maombolezo, lakini moyo wa wapumbavu uko katika nyumba ya karamu.
5Ni bora kusikiliza maonyo ya mtu mwenye hekima kuliko kusikiliza wimbo wa wapumbavu.
6Kwa kuwa kama mlio wa miiba chini ya chungu, ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu. Huu pia ni mvuke.
7kweli jeuri humfanya mtu mwenye hekima kuwa mpumbavu, na rusha huharibu moyo.
8Ni heri mwisho wa jambo kuliko mwanzo; na watu wenye uvumilivu ni bora kuliko wenye majivuno rohoni.
9Usikasirike haraka rohoni mwako, kwa sababu hasira hukaa katika mioyo ya wapumbavu.