Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 17:1-21 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 17:1-21 in Biblia Takatifu

1 Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonika ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi.
2 Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akatumia Maandiko Matakatifu.
3 Aliyaeleza na kuonyesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka wafu. Akawaambia, “Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo.”
4 Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao.
5 Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani.
6 Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: “Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini.
7 Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu.”
8 Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu.
9 Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao.
10 Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi.
11 Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonika. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli.
12 Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.
13 Lakini, Wayahudi wa Thesalonika walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu.
14 Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea.
15 Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo.
16 Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu.
17 Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano sokoni pamoja na wowote wale waliojitokeza.
18 Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, “Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?” Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, “Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni.”
19 Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, “Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia.
20 Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani.”
21 Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya.
Matendo 17 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 17:1-21 in Biblia ya Kiswahili

1 Na walipopita katika miji ya Amfipoli na Apolonia, walikuja mpaka mji wa Thesalonike ambao kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2 Kama ilivyo kawaida ya Paulo, alienda kwao, na kwa muda wa siku tatu za Sabato alijadiliana nao juu ya maandiko.
3 Alikuwa akiwafungulia maandiko na kuwaeleza kuwa, ilimpasa Kristo ateseke na kisha kufufuka tena kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Kristo”
4 Baadhi ya Wayahudi walishawishika na kuungana na Paulo na Sila, pamoja na Wagiriki wachamungu, akinamama wengi waongofu na kundi kubwa la watu.
5 Lakini baadhi ya Wayahudi wasioamini, waliojawa na wivu, walienda sokoni na kuwachukuwa baadhi ya watu waovu, wakakusanya umati wa watu pamoja, na kusababisha ghasia mjini, kisha wakaivamia nyumba ya Jason, wakitaka kuwakamata Paulo na Sila ilikuwaleta mbele za watu.
6 Lakini walipowakosa, walimkamata Yasoni na baadhi ya ndugu wengine na kuwapeleka mbele ya maofisa wa mji, wakipiga kelele, “Hawa wanaume walioupindua ulimwengu wamefika mpaka huku pia,
7 Wanaume hawa waliokaribishwa na Yasoni wanaihalifu sheria ya Kaisari, wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu”
8 Umati na maofisa wa mji waliposikia mambo hayo, waliingiwa na wasiwasi.
9 Baada ya kuwa wamekwisha kuchukua fedha ya thamani ya ulinzi kutoka kwa Yason na wengine, waliwaachia waende.
10 Usiku ule ndugu walimtuma Paulo na Sila Beroya. Na walipofika kule walikwenda katika sinagogi la Wayahudi.
11 Watu wale walikuwa wenye werevu mkubwa kuliko wale watu wa Thesalonike, kwa sababu walikuwa na utayari wa kulipokea neno kwa akili zao, na kuchunguza maandiko kila siku ili kuona kama maneno yaliyonenwa ndivyo yalivyo.
12 Kwa hiyo wengi wao waliamini, wakiwemo wanawake wenye ushawishi mkubwa wa Kigiriki na wanaume wengi.
13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo anatangaza neno la Mungu huko Beroya, walienda huko na kuchochea na kisha kuanzisha ghasia kwa watu.
14 Kwa haraka, ndugu wakampeleka Paulo kwa njia ya ziwa, lakini Sila na Timotheo wakabaki pale.
15 Wale ndugu waliompeleka Paulo walienda naye hadi Athene, walipomwacha Paulo huko, walipokea maagizo kutoka kwake kuwa, Sila na Timotheo waje kwake kwa haraka iwezeanavyo.
16 Na wakati akiwasubiri huko Athene, roho yake ilikasirishwa ndani yake kwa jinsi alivyouona mji ulivyojaa sanamu nyingi.
17 Hivyo akajadiliana katika sinagogi na wayahudi wale waliomcha Mungu na kwa wale wote aliokutana nao kila siku sokoni.
18 Lakini baathi ya Wanafalsafa wa Waepikureo na Wastoiko wakamkabili. Na wengine wakasema, “Ni nini anachokisema huyu mwongeaji mchanga? Wengine wakasema, “inaonekana anahubiri habari ya mungu mgeni,” kwasababu anahubiri habari ya Yesu na ufufuo.
19 Wakamchukua Paulo na kumleta Areopago, wakisema, “Twaweza kujua haya mafundisho mapya unayoyaongea?
20 Kwasababu unaleta mambo mapya katika masikio yetu. Kwahivyo tunataka kujua haya mambo yana maana gani?”
21 (Na watu wote wa Athene pamoja na wageni waliopo kwao, hutumia muda wao aidha katika kuongea na kusikiliza juu ya jambo jipya.)
Matendo ya Mitume 17 in Biblia ya Kiswahili