4 Watu wa mji huo waligawanyika: wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume.
5 Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe.
6 Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani,
7 wakawa wanahubiri Habari Njema huko.
8 Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa amelemaa miguu tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe.
9 Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa,
10 akasema kwa sauti kubwa, “Simama wima kwa miguu yako!” Huyo mtu aliyelemaa akainuka ghafla, akaanza kutembea.
11 Umati wa watu walipoona alichofanya Paulo, ulianza kupiga kelele kwa lugha ya Kilukaonia: “Miungu imetujia katika sura za binadamu!”
12 Barnaba akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme.
13 Naye kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua mbele ya mlango mkuu wa mji, na pamoja na ule umati wa watu akataka kuwatambikia mitume.