Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 23:1-19 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 23:1-19 in Biblia Takatifu

1 Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, “Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu.”
2 Hapo Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni.
3 Basi, Paulo akamwambia, “Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja Sheria kwa kuamuru nipigwe?”
4 Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, “Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu!”
5 Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni Kuhani Mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.”
6 Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaaza sauti yake mbele ya Baraza: “Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka.”
7 Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili.
8 Kisa chenyewe kilikuwa hiki: Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu.
9 Kelele ziliongezeka na baadhi ya walimu wa Sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: “Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye.”
10 Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome.
11 Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, “Jipe moyo! Umenishuhudia katika Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma.”
12 Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.”
13 Watu zaidi ya arobaini ndio waliokula njama kufanya hivyo.
14 Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, “Sisi tumeapa kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo.
15 Sasa basi, ninyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumuua hata kabla hajafika karibu.”
16 Lakini mtoto wa kiume wa dada yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo.
17 Hapo Paulo akamwita mmoja wa askari, akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia.”
18 Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, “Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukwambia.”
19 Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, “Una nini cha kuniambia?”
Matendo 23 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 23:1-19 in Biblia ya Kiswahili

1 Paulo akawaangalia moja kwa moja watu wa baraza na kusema, “Ndugu zangu, nimeishi mbele za Mungu kwa dhamira nzuri hadi hivi leo.”
2 Kuhani mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.
3 Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Umekaa ukinihukumu kwa sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?”
4 Wale waliokuwa wamesimama karibu naye wakasema, “Hivi ndivyo unavyomtukana kuhani mkuu wa Mungu?”
5 Paulo akasema, “ndugu zangu, mimi sikujua kwamba huyu ni kuhani mkuu. Kwa kuwa imeandikwa, hutazungumza vibaya juu ya mtawala wa watu wako.”
6 Paulo alipoona ya kwamba upande mmoja wa baraza ni Masadukayo na wengine Mafarisayo, akapaza sauti na kusema, “ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Ni kwa sababu hii nategemea kwa ujasiri ufufuo wa wafu ninao hukumiwa nao.”
7 Alipoyasema haya, malumbano makubwa yakatokea baina ya Mafarisayo na Masadukayo, na mkutano ukagawanyika.
8 Kwani Masadukayo husema hakuna ufufuo, malaika wala hakuna roho, ila Mafarisayo husema haya yote yapo.
9 Ghasia kubwa ikatokea na baadhi ya waandishi waliokuwa upande wa Mafarisayo wakasimama na kujadili, wakisema, “hatujaona chochote kibaya dhidi ya mtu huyu. Vipi kama roho au malaika ameongea na yeye?”
10 Wakati kulitokea hoja kubwa, mkuu wa majeshi aliogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipande vipande na wao, hivyo akaamuru wanajeshi washuke chini na kumchukua kwa nguvu kutoka kwa wajumbe wa baraza, na kumleta katika ngome.
11 Usiku uliofuata Bwana alisimama karibu naye na kusema, “Usiogope, kwa kuwa umenishuhudia katika Yerusalemu, hivyo utatoa ushahidi pia katika Roma.”
12 Kulipokucha, baadhi ya Wayahudi walifanya agano na kuita laana juu yao wenyewe: walisema ya kwamba hawatakula wala kunywa chochote mpaka watakapomuua Paulo.
13 Kulikuwa na watu zaidi ya arobaini ambao walifanya njama hii.
14 wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejiweka wenyewe kwenye laana kuu, tusile chochote hadi tutakapomwua Paulo.
15 Hivyo sasa, baraza limwambie jemadari mkuu amlete kwenu, kana kwamba mnaamua kesi yake kwa usahihi. Kwetu sisi tuko tayari kumwua kabla hajaja hapa.”
16 Lakini mtoto wa dada yake na Paulo akasikia kwamba kulikuwa na njama, akaenda akaingia ndani ya ngome na kumwambia Paulo.
17 Paulo akamwita akida mmoja akasema, “Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwambia.”
18 Basi akida akamchukua yule kijana akampeleka kwa jemedari mkuu akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwako. Ana neno la kukuambia.”
19 Yule jemadari mkuu akamshika kwa mkono akajitenga naye kando, na akamwuliza, “Ni kitu gani unachotaka kuniambia?”
Matendo ya Mitume 23 in Biblia ya Kiswahili