Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 23

Matendo 23:1-19

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, “Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu.”
2Hapo Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni.
3Basi, Paulo akamwambia, “Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja Sheria kwa kuamuru nipigwe?”
4Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, “Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu!”
5Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni Kuhani Mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.”
6Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaaza sauti yake mbele ya Baraza: “Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka.”
7Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili.
8Kisa chenyewe kilikuwa hiki: Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu.
9Kelele ziliongezeka na baadhi ya walimu wa Sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: “Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye.”
10Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome.
11Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, “Jipe moyo! Umenishuhudia katika Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma.”
12Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.”
13Watu zaidi ya arobaini ndio waliokula njama kufanya hivyo.
14Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, “Sisi tumeapa kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo.
15Sasa basi, ninyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumuua hata kabla hajafika karibu.”
16Lakini mtoto wa kiume wa dada yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo.
17Hapo Paulo akamwita mmoja wa askari, akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia.”
18Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, “Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukwambia.”
19Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, “Una nini cha kuniambia?”

Read Matendo 23Matendo 23
Compare Matendo 23:1-19Matendo 23:1-19