10 Nikasema, 'Nifanye nini, Bwana?' Bwana akaniambia, 'Simama na uingie Dameski; huko utaambiwa kila kitu unachopaswa kufanya.'
11 Sikuweza kuona kwa sababu ya muangaza wa nuru ile, ndipo nikaenda Dameski kwa kuongozwa na mikono ya wale waliokuwa na mimi.
12 Huko nikakutana na mtu aitwaye Anania, alikuwa mtu aliyeshika sheria na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote walioishi huko.
13 Akaja kwangu, akasimama mbele yangu, na kusema, 'Ndugu yangu Sauli, upate kuona.' Kwa muda ule ule nikamuona.
14 Akasema, 'Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, kumuona yule mwenyehaki, na kusikia sauti itokayo kwenye kinywa chake.
15 Kwa sababu utakuwa shahidi kwake kwa watu wote juu ya uliyoyaona na kusikia.
16 Basi sasa kwa nini unasubiri? Amka, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliita jina lake.'
17 Baada ya kurejea Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, ikatokea kwamba nikapewa maono.
18 Nikamuona akiniambia, 'Hima na utoke Yerusalemu haraka, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu mimi.'
19 Nikasema, 'Bwana, wao wenyewe wanajua niliwafunga gerezani na kuwapiga wale waliokuamini katika kila sinagogi.
20 Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, Mimi pia nilikuwa nimesimama karibu na kukubali na nilikuwa nalinda nguo za wale waliomwua.'
21 Lakini aliniambia, 'Enenda, kwa sababu mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa mataifa.”'
22 Watu wakamruhusu aongee juu ya neno hili. Lakini baadaye walipaza sauti na kusema, “mwondoe mtu huyu katika nchi: kwa sababu sio sahihi aishi.”
23 Walipokuwa wakipaza sauti, na kutupa mavazi yao na kutupa mavumbi juu,
24 jemedari mkuu akaamuru Paulo aletwe ngomeni. Akaamuru aulizwe huku anapigwa mijeledi, ili yeye mwenyewe ajue kwa nini walikuwa wanampigia kelele namna ile.
25 Hata walipokuwa wamemfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliye simama karibu naye, “Je! ni haki kwenu kumpiga mtu aliye Mrumi na bado hajahukumiwa?”
26 Yule akida aliposikia maneno haya, akaenda kwa jemedari mkuu na kumwambia, akisema, “Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni mrumi.”
27 Jemedari mkuu akaja na kumwambia, “Niambie, je wewe ni raia wa Rumi?” Paulo akasema, “Ndiyo.”