Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 13:4-17 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 13:4-17 in Biblia Takatifu

4 Basi, Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia, na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro.
5 Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi. Yohane (Marko) alikuwa msaidizi wao.
6 Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo upande wa pili, na huko walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Baryesu ambaye alijisingizia kuwa nabii.
7 Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu.
8 Lakini huyo mchawi Elima (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo.
9 Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi,
10 akasema, “Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka.
11 Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo.” Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze.
12 Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.
13 Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu.
14 Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa.
15 Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: “Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni.”
16 Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: “Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni!
17 Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu.
Matendo 13 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 13:4-17 in Biblia ya Kiswahili

4 Kwa hiyo Barnabas na Sauli walimtii Roho Mtakatifu na walitelemka kuelekea Seleukia; Kutoka huko walisafiri baharini kuelekea kisiwa cha Kipro.
5 Walipokuwa katika mji wa Salami, walilitangaza neno la Mungu katika Masinagogi ya Wayahudi. Pia walikuwa pamoja na Yohana Marko kama msaidizi wao.
6 Walipokwenda katika kisiwa chote mpaka Pafo, walikuta mtu fulani mchawi, Myahudi nabii wa uongo, ambaye jina lake lilikuwa Bar Yesu.
7 Mchawi huyu alishirikiana na Liwali Sergio Paulus, aliyekuwa mtu mwenye akili. Mtu huyu aliwaalika Barnaba na Sauli, kwa sababu alihitaji kusikia neno la Mungu.
8 Lakini Elima “yule mchawi” (hivyo ndivyo jina lake lilivyo tafsiriwa) aliwapinga; alijaribu kumgeuza yule liwali atoke kwenye imani.
9 Lakini Sauli aliyeitwa Paulo, alikuwa amejazwa na Roho Mtakatikfu, akamkazia macho
10 na akasema “Ewe mwana wa Ibilisi, umejazwa na aina zote za udanganyifu na udhaifu. Wewe ni adui wa kila aina ya haki. Hautakoma kuzigeuza njia za Bwana, zilizonyooka, je utaweza?
11 Sasa tazama, mkono wa Bwana upo juu yako, na utakuwa kipofu. Hautaliona Jua kwa muda” mara moja ukungu na giza vilianguka juu ya Elimas; alianza kuzunguka pale akiomba watu wamwongoze kwa kumshika mkono.
12 Baada ya liwali kuona kilichotokea, aliamini, kwa sababu alishangazwa kwa mafundisho kuhusu Bwana.
13 Sasa Paulo na rafiki zake walisafiri majini kutoka Pafo na wakafika Perge katika Pamfilia. Lakini Yohana aliwaacha na kurudi Yerusalemu.
14 Paulo na rafiki yake walisafiri kutoka Perge na wakafika Antiokia ya Pisidia. Huko walikwenda katika sinagogi siku ya Sabato na kukaa chini.
15 Baada ya kusoma sheria na manabii, viongozi wa sinagogi aliwatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mnao ujumbe wa kutia moyo watu hapa, semeni”
16 Kwa hiyo Paulo alisimama na kuwapungia mkono; alisema, “Wanaume wa Israeli na enyi mnao mtii Mungu, sikilizeni.
17 Mungu wa hawa watu wa Israeli aliwachagua baba zetu na kuwafanya watu wengi walipokaa katika nchi Misri, na kwa mkono wake kuinuliwa aliwaongoza nje yake.
Matendo ya Mitume 13 in Biblia ya Kiswahili