Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Matendo - Matendo 13

Matendo 13:4-17

Help us?
Click on verse(s) to share them!
4Basi, Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia, na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro.
5Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi. Yohane (Marko) alikuwa msaidizi wao.
6Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo upande wa pili, na huko walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Baryesu ambaye alijisingizia kuwa nabii.
7Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu.
8Lakini huyo mchawi Elima (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo.
9Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi,
10akasema, “Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka.
11Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo.” Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze.
12Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.
13Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu.
14Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa.
15Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: “Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni.”
16Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: “Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni!
17Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu.

Read Matendo 13Matendo 13
Compare Matendo 13:4-17Matendo 13:4-17