6 kwa kuwa rafiki yangu amepitia kwangu akiwa safarini nami sina cha kumpa.
7 Naye, akiwa ndani angemjibu: Usinisumbue! Nimekwisha funga mlango. Mimi na watoto wangu tumelala; siwezi kuamka nikupe!
8 Hakika, ingawa hataamka ampe kwa sababu yeye ni rafiki yake, lakini, kwa sababu ya huyo mtu kuendelea kumwomba, ataamka ampe chochote anachohitaji.
9 Kwa hiyo, ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa.
10 Maana yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata na abishaye hufunguliwa.
11 Mtoto akimwomba baba yake samaki, je, atampa nyoka badala ya samaki?
12 Na kama akimwomba yai, je, atampa ng'e?
13 Ninyi, ingawa ni waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Basi, baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi; atawapa Roho Mtakatifu wale wanaomwomba.”
14 Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea hata umati wa watu ukashangaa.
15 Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anamfukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.”
16 Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonyesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni.
17 Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliofarakana wenyewe, hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yeyote inayofarakana huangamia.