Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Luka 11:21-48 in Swahili (individual language)

Help us?

Luka 11:21-48 in Biblia Takatifu

21 “Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama.
22 Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara.
23 Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
24 “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu fulani, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzikia. Asipopata, hujisemea: Nitarudi kwenye makao yangu nilikotoka.
25 Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa.
26 Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba waovu zaidi kuliko yeye; wote huenda na kumwingia mtu yule. Hivyo, basi hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko pale mwanzo.”
27 Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri tumbo lililokuzaa, na maziwa yaliyokunyonyesha!”
28 Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”
29 Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
30 Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.
31 Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atashuhudia kwamba kina hatia. Yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni; kumbe hapa pana mkuu zaidi kuliko Solomoni.
32 Watu wa Ninewi watatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, na watashuhudia kwamba kizazi hiki kina hatia. Hao watu wa Ninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na hapa pana mkuu zaidi kuliko Yona!
33 “Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa pishi, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga.
34 Jicho lako ni kama taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza.
35 Uwe mwangalifu basi mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.
36 Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utang'aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.”
37 Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula.
38 Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa.
39 Bwana akamwambia, “Ninyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu.
40 Wapumbavu ninyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia?
41 Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu.
42 “Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine.
43 “Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani.
44 Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.”
45 Mmoja wa walimu wa Sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.”
46 Yesu akamjibu, “Na ninyi walimu wa Sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku ninyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia.
47 Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua.
48 Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao.
Luka 11 in Biblia Takatifu

Luka 11:21-48 in Biblia ya Kiswahili

21 Mtu mwenye nguvu aliye na silaha akilinda nyumba yake, vitu vyake vitakaa salama.
22 Lakini akivamiwa na mtu mwenye nguvu zaidi, Yule mtu mwenye nguvu atamnyang'anya silaha zake, na kuzichukua mali zake zote.
23 Yeye asiye pamoja nami yuko kinyume nami, na yeye asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
24 Pepo mchafu amtokapo mtu, huenda na kutafuta mahali pasipo na maji ili ajipumzishe. Atakapokuwa amekosa, husema, 'nitarudi nilipotoka.
25 Akirudi na kukuta nyumba imefagiliwa na imekaa vizuri.
26 Hivyo huenda na kutafuta mapepo saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe na kuwaleta waje wakae mahali pale. Na hali ya mtu huyo huwa mbaya kuliko ilivyokuwa mara ya kwanza.”
27 Ilitokea kwamba alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke fulani alipasa sauti yake zaidi ya wote kwanye mkutano wa watu na kusema “Limebarikiwa tumbo lililo kuzaa na matiti uliyoyanyonya”
28 Lakini yeye akasema, wamebarikiwa wale wasikio neno la Mungu na kulitunza.
29 Wakati umati wa watu wanakusanyika na kuongezeka, Yesu akaanza kusema “Kizazi hiki ni kizazi cha uovu. Hutafuta ishara, na hakuna ishara watayopewa zaidi ya ile ishara ya Yona.
30 Maana kama Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki
31 Malkia wa Kusini atasimama siku ya hukumu na watu wa kizazi hiki na kuwahukumu wao, kwani yeye alitoka katika mwisho wa nchi ili aje asikilize hekima za Solomoni, na hapa yuko aliye mkuu kuliko Solomoni.
32 Watu wa Ninawi watasimama katika hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki siku ya hukumu watakihukumu, kwani wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na tazama, hapa yuko aliye mkuu kuliko Yona.
33 Hakuna Mtu yeyote, awashaye taa na kuiweka sehemu ya chini yenye giza isiyoonekana au chini ya kikapu, ila huwasha na kuweka juu ya kitu ili kila mtu aingiaye aweze kuona mwanga.
34 Jicho lako ni taa ya mwili. Jicho lako likiwa zuri basi mwili wako wote utakuwa kwenye mwanga. Lakini jicho lako likiwa baya basi mwili wako wote utakuwa kwenye giza.
35 Kwa hiyo, mjihadhari ili mwanga ulio ndani yenu usitiwe giza.
36 Hivyo basi, kama mwili wako wote uko kwenye mwanga, na hakuna sehemu iliyo katika giza, basi mwili wako utakuwa sawa na taa iwakayo na kutoa mwanga kwenu.”
37 Alipomaliza kuongea, Farisayo alimwalika akale chakula nyumbani kwake, naye Yesu akaingia ndani na kuwa pamoja nao.
38 Na Mafarisayo wakashangaa kwa jinsi ambavyo hakunawa kwanza kabla ya chakula cha jioni.
39 Lakini Bwana akawaambia, “Ninyi Mafarisayo mnaosha nje ya vikombe na bakuli, lakini ndani yenu mmejaa tamaa na uovu.
40 Ninyi watu msio na ufahamu, Je yeye aliyeumba nje hakuumba na ndani pia?
41 Wapeni masikini yaliyo ndani, na mambo yote yatakuwa safi kwenu.
42 Lakini ole wenu Mafarisayo, kwani mnatoa zaka ya mnanaa na mchicha na kila aina ya mboga ya bustani. Lakini mmeacha mambo ya haki na kumpenda Mungu. Ni muhimu zaidi kufanya yaliyo ya haki na kumpenda Mungu, bila kuacha kufanya na hayo mengine pia.
43 Ole wenu Mafarisayo, kwa kuwa mnapenda kukaa katika viti vya mbele kwenye masinagogi na kuamkiwa kwa salamu za heshima sokoni.
44 Ole wenu, kwani mnafanana na makaburi yasiyo na alama ambayo watu hutembea juu yake pasipokujua.”
45 Mwalimu mmoja wa sheria za Kiyahudi akamjibu na kumwambia, “Mwalimu, unachokisema kinatuudhi pia sisi.”
46 Yesu akasema, “Ole wenu, waalimu wa sheria! kwani mnawapa watu mizigo mikubwa wasiyoweza kuibeba, walakini ninyi hamgusi mizigo hiyo hata kwa moja ya vidole vyenu.
47 Ole wenu, kwa sababu mnajenga na kuweka kumbukumbu kwenye makaburi ya manabii' ambao waliuwawa na mababu zenu.
48 Hivyo ninyi mwashuhudia na kukubaliana na kazi walizozifanya mababu zenu, kwa sababu hakika waliwauwa manabii ambao mnajenga kumbukumbu katika makaburi yao.
Luka 11 in Biblia ya Kiswahili