Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 11

Luka 11:21-48

Help us?
Click on verse(s) to share them!
21“Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama.
22Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara.
23Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
24“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu fulani, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzikia. Asipopata, hujisemea: Nitarudi kwenye makao yangu nilikotoka.
25Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa.
26Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba waovu zaidi kuliko yeye; wote huenda na kumwingia mtu yule. Hivyo, basi hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko pale mwanzo.”
27Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri tumbo lililokuzaa, na maziwa yaliyokunyonyesha!”
28Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”
29Umati wa watu ulipozidi kuongezeka, Yesu akawaambia, “Kizazi hiki ni kizazi kiovu. Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
30Jinsi Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninewi, ndivyo pia Mwana wa Mtu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.
31Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atashuhudia kwamba kina hatia. Yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni; kumbe hapa pana mkuu zaidi kuliko Solomoni.
32Watu wa Ninewi watatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, na watashuhudia kwamba kizazi hiki kina hatia. Hao watu wa Ninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona; na hapa pana mkuu zaidi kuliko Yona!
33“Hakuna mtu anayewasha taa na kuifunika kwa pishi, bali huiweka juu ya kinara ili watu wanaoingia ndani wapate kuona mwanga.
34Jicho lako ni kama taa ya mwili wako; likiwa zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga. Jicho lako likiwa bovu, na mwili wako pia utakuwa katika giza.
35Uwe mwangalifu basi mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.
36Basi, kama mwili wako wote una mwanga, bila kuwa na sehemu yoyote yenye giza, mwili huo utang'aa kikamilifu kama vile taa inavyokuangazia kwa mwanga wake.”
37Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula.
38Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa.
39Bwana akamwambia, “Ninyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu.
40Wapumbavu ninyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia?
41Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu.
42“Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine.
43“Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani.
44Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.”
45Mmoja wa walimu wa Sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.”
46Yesu akamjibu, “Na ninyi walimu wa Sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku ninyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia.
47Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua.
48Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao.

Read Luka 11Luka 11
Compare Luka 11:21-48Luka 11:21-48