Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - 2 Wakorintho

2 Wakorintho 6

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure.
2Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu!
3Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote.
4Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.
5Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula.
6Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,
7kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto.
8Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli;
9kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa.
10Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.
11Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa.
12Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu.
13Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.
14Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja?
15Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini?
16Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: “Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”
17Kwa hiyo Bwana asema pia: “Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea.
18Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo.”