1Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu.
2Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia.
3Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo yesu.
4Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi.
5Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo.
6Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno.
7Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uyaelewe yote.
8Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri.
9Kwa sababu ya kuihubiri Habari Njema mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo,
10na hivyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele.
11Usemi huu ni wa kweli: “Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye.
12Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana.
13Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe.”
14Basi, wakumbushe watu wako mambo haya, na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia.
15Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake, na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli.
16Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu.
17Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto.
18Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika.
19Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.”
20Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine ni vya matumizi ya pekee na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
21Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema.
22Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi.
23Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi.
24Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu,
25ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli.
26Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.