6 Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.
7 Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.”
8 Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini.
9 Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
10 Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”
11 Huyo mwanamke akamjibu, “Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”
12 Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima.”
13 Basi, Mafarisayo wakamwambia, “Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali.”
14 Yesu akawajibu, “Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
15 Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
16 Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.
17 Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.”
19 Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu “Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”
20 Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
21 Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika.”
22 Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: Niendako ninyi hamwezi kufika?”
23 Yesu akawaambia, “Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24 Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba Mimi ndimi, mtakufa katika dhambi zenu.”
25 Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo!
26 Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.”
27 Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.