Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Yohana 8:1-48 in Swahili (individual language)

Help us?

Yohana 8:1-48 in Biblia Takatifu

1 lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.
2 Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha.
3 Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.
4 Kisha wakamwuliza Yesu, “Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.
5 Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?”
6 Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.
7 Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.”
8 Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini.
9 Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
10 Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”
11 Huyo mwanamke akamjibu, “Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”
12 Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima.”
13 Basi, Mafarisayo wakamwambia, “Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali.”
14 Yesu akawajibu, “Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
15 Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
16 Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.
17 Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.”
19 Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu “Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”
20 Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
21 Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika.”
22 Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: Niendako ninyi hamwezi kufika?”
23 Yesu akawaambia, “Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24 Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba Mimi ndimi, mtakufa katika dhambi zenu.”
25 Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo!
26 Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.”
27 Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.
28 Basi, Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba Mimi ndimi, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.
29 Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza.”
30 Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.
31 Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
32 Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.”
33 Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: mtakuwa huru?”
34 Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35 Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.
36 Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.
37 Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu.
38 Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”
39 Wao wakamjibu, “Baba yetu ni Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
40 Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
41 Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.”
42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43 Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
44 Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
45 Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
46 Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?
47 Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu.”
48 Wayahudi wakamwambia, “Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?”
Yohana 8 in Biblia Takatifu

Yohana 8:1-48 in Biblia ya Kiswahili

1 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Yesu alienda mlima wa Mizeituni.
2 Mapema asubuhi akaja tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; akakaa na kuwafundisha.
3 Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyekamatwa katika kitendo cha kuzini. Wakamweka katikati.
4 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Ndipo wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa katika uzinzi, katika kitendo kabisa.
5 Sasa, katika sheria, Musa ametuamuru kuwaponda mawe watu kama hawa, unasemaje juu yake?
6 Walisema haya ili kumtega ili kwamba wapate jambo la kumshitaki, lakini Yesu akainama chini akaandika katika ardhi kwa kidole chake.
7 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Walipoendelea kumwuliza, alisimama na kuwaambia, “Yeye asiyekuwa na dhambi miongoni mwenu, awe wa kwanza kumponda mawe.”
8 Akainama tena chini, akaandika katika ardhi kwa kidole chake.
9 (Zingatia: Angalia ufafanuzi wa Yohana 7: 53 - 8: 11 hapo juu). Waliposikia hayo, waliondoka mmoja baada ya mwingine, kuanzia aliye mzee. Mwishowe Yesu aliachwa peke yake, pamoja na mwanamke aliyekuwa katikati yao.
10 Yesu alisimama na kumwambia, “Mwanamke, waliokushitaki wako wapi? Hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”
11 Akasema, “Hakuna hata mmoja Bwana.” Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda njia yako; kuanzia sasa na kuendelea usitende dhambi tena.”
12 Tena Yesu akazungumza na watu akisema, “Mimi ni nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hatatembea gizani bali atakuwa na nuru ya uzima.”
13 Mafarisayo wakamwambia, “Unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako siyo wa kweli.”
14 Yesu alijibu akawaambia, “Hata kama nitajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli. Ninajua mahali nilikotoka na kule ninakoenda, lakini ninyi hamjui mahali ninapotoka au kule ninakoenda.
15 Nyinyi mnahukumu kimwili; mimi simhukumu yeyote.
16 Mimi hata nikihukumu, hukumu yangu ni kweli kwa sababu siko peke yangu, bali niko pamoja na baba aliyenituma.
17 Ndiyo, na katika sheria yenu imeandikwa kwamba ushuhuda wa watu wawili ni kweli.
18 Mimi ndiye ninayejishuhudia, na Baba aliyenituma ananishuhudia.”
19 Wakamwambia, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akajibu, “mimi hamnijui wala Baba yangu hammjui; mngelikuwa mnanijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”
20 Alisema maneno haya akiwa karibu na hazina alipokuwa akifundisha hekaluni, na hakuna hata mmoja aliyemkamata kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijafika.
21 Basi akawaambia tena, “Ninaenda zangu; mtanitafuta na mtakufa katika dhambi zenu. Kule niendako, hamuwezi kuja.”
22 Wayahudi wakasema, “Atajiua mwenyewe, yeye ambaye alisema, 'kule niendako hamuwezi kuja'?”
23 Yesu akawaambia, “Mnatoka chini; mimi natoka juu. Ninyi ni wa Ulimwengu huu; mimi si wa ulimwengu huu.
24 Kwa hiyo, naliwaambieni kuwa mtakufa katika dhambi zenu. Vinginevyo muamini kuwa MIMI NDIYE, mtakufa katika dhambi zenu”.
25 Kwa hiyo wakamwambia, “Wewe ni nani?” Yesu akawaambia, Yale niliyowaambia tangu mwanzo.
26 Ninayo mambo mengi ya kuzungumza na kuhukumu juu yenu. Hata hivyo, yeye aliyenituma ni wa kweli; na mambo niliyoyasikia kutoka kwake, mambo haya nayasema kwa Ulimwengu.”
27 Hawakumuelewa kwamba alikuwa akiongea nao kuhusu Baba.
28 Yesu akasema, “Mtakapomwinua juu Mwana wa Mtu, ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE, na kwamba sifanyi lolote kwa nafsi yangu. Kama Baba alivyonifundisha, ninazungumza mambo haya.
29 Yeye aliyenituma yuko pamoja nami, na yeye hajaniacha peke yangu, kwani kila mara nafanya yale yanayompendeza.”
30 Wakati Yesu akisema mambo haya, wengi walimwamini.
31 Yesu akasema kwa wale Wayahudi waliomwamini, “Ikiwa mtakaa katika neno langu, ndipo mtakuwa wanafunzi wangu kweli,
32 nanyi mtaijua kweli, na kweli itawaweka huru.”
33 Walimjibu, “Sisi ni uzao wa Ibrahimu na kamwe hatujawahi kwa chini ya utumwa wa yeyote; utasemaje, “Tutawekwa huru?”
34 Yesu aliwajibu, “Amini, amini, nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35 Mtumwa hakai nyumbani wakati wote; mwana hudumu siku zote.
36 Kwa hiyo, ikiwa Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kabisa.”
37 Ninajua kwamba ninyi ni uzao wa Ibrahimu; mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halina nafasi ndani yenu.
38 Ninasema mambo ambayo nimeyaona pamoja na Baba yangu, na ninyi vile vile mnafanya mambo ambayo mliyasikia kutoka kwa baba yenu.”
39 Walijibu na kumwambia, “Baba yetu ni Abrahamu.” Yesu akawaambia, Kama mngelikuwa watoto wa Ibrahimu, mngefanya kazi za Ibrahimu.
40 Hata sasa mnatafuta kuniua, mtu aliyewaambia ukweli kwamba nilisikia kutoka kwa Mungu. Abrahamu hakufanya hivi.
41 Mnafanya kazi za baba yenu.” Wakamwambia, “Hatukuzaliwa katika uzinzi, tunaye Baba mmoja, Mungu.”
42 Yesu akawaambia, “Ikiwa Mungu ni Baba yenu, mngenipenda mimi, kwa maana nimetoka kwa Mungu; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye alinituma.
43 Kwa nini hamyaelewi maneno yangu? Kwa sababu hamuwezi kuvumilia kuyasikia maneno yangu.
44 Ninyi ni wa baba yenu, shetani, na mnataka kuzitenda tamaa za baba yenu. Alikuwa mwuaji tangu mwanzo na hawezi kusimama katika kweli kwa sababu kweli haimo ndani yake. Anapoongea uongo, anaongea kutoka kwenye asili yake kwa sababu ni mwongo na baba wa uongo.
45 Hata sasa, kwa sababu ninasema iliyo kweli, hamniamini.
46 Ni nani kati yenu anayenishuhudia kuwa nina dhambi? ikiwa ninasema iliyo kweli, kwa nini hamniamini?
47 Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; ninyi hamyasikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.”
48 Wayahudi wakamjibu na kumwambia, hatujasema kweli kuwa wewe ni Msamaria na una pepo?”
Yohana 8 in Biblia ya Kiswahili