48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
50 Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa.
51 Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
52 Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao:
53 Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu.
54 Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake.
57 Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu.
58 Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zetu, wakafa. Aulaye mkate huu ataishi milele.”
59 Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.
60 Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, “Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?”
61 Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananung'unika juu ya jambo hilo, akawauliza, “Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka?
62 Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza?
63 Roho ndiye atiaye uzima; binadamu peke yake hawezi. Maneno niliyowaambieni ni Roho, ni uzima.
64 Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini.” (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti.)
65 Kisha akasema, “Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu.”
66 Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma wasiandamane naye tena.
67 Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo uzima wa milele.
69 Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu.”
70 Yesu akawaambia, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!”