40 Kwa kuwa haya ndiyo mapenzi ya Baba yangu, kwamba yeyote amtazamaye Mwana na kumwamini apate uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
41 Kisha wayahudi wakamnung`unikia kumhusu yeye kwa sababu alisema, “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
42 Wakasema, “Huyu siyo Yesu mwana wa Yusuph, ambaye baba yake na mama yake tunamfahamu? Imekuwaje sasa anasema, 'Nimeshuka kutoka mbinguni`?”
43 Yesu akajibu, akawambia, “Msinung'unikiane miongoni mwenu wenyewe.
44 Hakuna mtu ajaye kwangu asipovutwa na Baba yangu aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.
45 Kwa kuwa imeandikwa katika manabii, 'Watafundishwa na Mungu.' Kila aliyesikia na amejifunza kutoka kwa Baba, huja kwangu.
46 Sio kwamba kuna mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu- amemwona Baba.
47 Amini, amini yeye aaminiye anao uzima wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 mababa zenu walikula manna jangwani, na wakafa.
50 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, ili kwamba mtu aule sehemu yake ili asife.
51 Mimi ni mkate uishio ambao umeshuka kutoka mbinguni. Kama mtu yeyote akila sehemu ya mkate huu, ataishi milele. Mkate nitakao utoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
52 Wayahudi wakakasirika wenyewe kwa wenyewe na wakaanza kubishana wakisema, “Mtu huyu anawezaje kutupa mwili wake tuule?”
53 Kisha Yesu akawambia, “Amini, amini, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamta kuwa na uzima ndani yenu.
54 Yeyote aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa kuwa mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Yeye aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami ndani yake.
57 Kama Baba mwenye uzima alivyonituma, na kama niishivyo kwa sababu ya Baba, na yeye pia ataishi kwa sababu yangu.