25 Baada ya kumpata upande mwingine wa ziwa wakamuuliza, “Rabbi ulikuja lini huku?”
26 Yesu akawajibu, akawambia, Amini, amini, mnanitafuta mimi, sio kwa sababu mliziona ishara, bali kwa sababu mlikula mikate na kushiba.
27 Acheni kukifanyia kazi chakula chenye kuharibika, bali mkifanyie kazi chakula kidumucho hata milele kile ambacho mwana wa Adamu atawapa, kwa kuwa Mungu Baba ameweka muhuri juu yake.”
28 Kisha wakamwambia, “Ni nini tunapaswa kufanya ili kuzifanya kazi za Mungu?”
29 Yesu akajibu, “Hii ndiyo kazi ya Mungu: kwamba mmwamini yeye aliyemtuma.”
30 Basi wakamwambia, “Ni ishara zipi utakazofanya, kwamba tunaweza kuziona na kukuamini? Utafanya nini?
31 Baba zetu walikula manna jangwani, kama ilivyo andikwa, “Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.”
32 Kisha Yesu akawajibu, “Amini, amini, sio Musa aliyewapa mkate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye awapaye mkate wa kweli kutoka mbinguni.
33 Kwa kuwa mkate wa Mungu ni ule ushukao kutoka mbinguni na kuupatia uzima ulimwengu.
34 Basi wakamwambia, “Bwana tupatie huu mkate wakati wote.”
35 Yesu akawambia, “Mimi ndiye mkate wa uzima, yeye ajaye kwangu hatapata njaa na yeye aniaminiye hatahisi kiu kamwe.”
36 Ingawa niliwaambia kwamba, mmeniona, na bado hamuamini.
37 Wote ambao Baba anaonipa watakuja kwangu, na yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kabisa.
38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni, sio kwa ajili ya kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma.
39 Na haya ndiyo mapenzi yake aliyenituma, kwamba nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali nitawafufua siku ya mwisho.
40 Kwa kuwa haya ndiyo mapenzi ya Baba yangu, kwamba yeyote amtazamaye Mwana na kumwamini apate uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
41 Kisha wayahudi wakamnung`unikia kumhusu yeye kwa sababu alisema, “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
42 Wakasema, “Huyu siyo Yesu mwana wa Yusuph, ambaye baba yake na mama yake tunamfahamu? Imekuwaje sasa anasema, 'Nimeshuka kutoka mbinguni`?”
43 Yesu akajibu, akawambia, “Msinung'unikiane miongoni mwenu wenyewe.
44 Hakuna mtu ajaye kwangu asipovutwa na Baba yangu aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.
45 Kwa kuwa imeandikwa katika manabii, 'Watafundishwa na Mungu.' Kila aliyesikia na amejifunza kutoka kwa Baba, huja kwangu.
46 Sio kwamba kuna mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu- amemwona Baba.
47 Amini, amini yeye aaminiye anao uzima wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 mababa zenu walikula manna jangwani, na wakafa.
50 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, ili kwamba mtu aule sehemu yake ili asife.
51 Mimi ni mkate uishio ambao umeshuka kutoka mbinguni. Kama mtu yeyote akila sehemu ya mkate huu, ataishi milele. Mkate nitakao utoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”